Serikali zafungua shughuli,WHO yaonya kuhusu wimbi la pili
12 Mei 2020Wakati shughuli zimeanza kufunguliwa tena katika nchi mbali mbali shirika la afya ulimwenguni WHO linaonya kuhusu hatari ya wimbi la pili la maambukizi.
Marekani imeingia siku ya pili ikiwa na vifo vichache ambapo ni watu 900 waliofariki, wakati shirika la afya ulimwenguni WHO likisifu hatua za maendeleo zilizopigwa duniani lakini limeonya kuwa na haja ya kuchukua tahadhari ya hali ya juu, dhidi ya kile ilichosema kuwa ni wimbi la pili la maambukizi.
Matumaini yamechafuliwa na hali mbaya inayoongezeka ya uchumi, ambapo Ufaransa inaonesha kuanguka kwa kiasi kikubwa kwa shughuli mwezi uliopita na kuonya kuwa shirika kubwa la ndege la Marekani huenda likafilisika kwasbabu ya janga hili, huku nafasi za kazi zikipotea na biashara kuporomoka.
Kiwango cha maambukizi katika nchi nyingi kimeanza kupungua, shirika la afya ulimwenguni WHO limeeleza, mbapo wiki kadhaa za kuwazuwia watu kutoka nje zimezaa matunda.
Wimbi la pili la maambukizi
"Taarifa nzuri ni kwamba kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza kasi ya maambukizi na hatimaye kuokoa maisha," mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliuambia mkutano kwa njia ya vidio.
Lakini shirika hilo la afya ulimwenguni limeonya kuhusu kutokea kwa wimbi la pili la maambukizi, ambapo mkuu wa kitengo cha dharura Michael Ryan amelalamika kwamba baadhi ya serikali zinachagua "kutembea kama vipofu" kwa kutoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na kufuatilia watu waliokutana na wale walioambukizwa.
Virusi vinaonekana kuingia katika Ikulu ya Marekani ya White House mwishoni mwa juma, ambapo kumekuwa na mtu wa pili aliyethibitishwa kuwa na virusi hivyo. Wafanyakazi katika Ikulu ya White House wameamriwa kuvaa barakoa kazini, na rais Donald Trump amesema huenda akapunguza kukaribiana na watu baada ya msaidizi wa makamu wa rais Mike Pence kugundulika kuwa ana virusi vya corona.
Mtandao wa reli nchini India unanza kufanyakazi leo wakati nchi hiyo taratibu ikiondoa hatua za kuwazuwia watu kutoka majumbani mwao , licha ya kuwa maambukizi mapya yanaongezeka.
Nchi hiyo yenye wakaazi bilioni 1.3 iliweka hatua kali za kuwataka watu kutotoka nje mwishoni mwa mwezi Machi, wakati serikali ya waziri mkuu Narendra Modi imsifiwa kwa kufanikiwa kubakisha idadi ya walioambukizwa kuwa 70,000, na vifo 2,000, tu.
Japan imethibitisha kuwa na kesi mpya za maambukizi 28 leo, ikiwa ni siku ya saba mfululizo ambapo idadi ya kila siku imebakia chini ya watu 40.