1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali za Tanzania, Kenya na Uganda zawasilisha bajeti kuu

Sylvia Mwehozi
11 Juni 2020

Mawaziri wa fedha wa Tanzania, Kenya na Uganda siku ya Alhamis waliwasilisha bajeti kuu za serikali kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 huku janga la virusi vya corona likiathiri uchumi.

https://p.dw.com/p/3deKz
Dr. Philip Mpango
Picha: DW/S. Khamis

Bungeni Dodoma

Wizara ya fedha nchini Tanzania imewasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2020-2021, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 34.87 kinatarajiwa kuidhinishwa kwa ajili ya maendeleo. 

Bajeti hii ambayo ni ya tano chini ya serikali ya awamu ya tano iliwasilishwa kwa mujibu wa ibara ya 137 ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na marekebisho yake na kifungu cha 29 sheria ya bajeti katika sura ya 39, inaonesha upekee katika ukuaji wa uchumi huku ikizingatia huduma za jamii.

Akionesha mafanikio ya bajeti iliopita kwa mwaka wa fedha 2019-2020 waziri mwenye dhamana ya fedha na mipango Dokta Philip Mpango amesema, upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya huduma ya maji safi na salama pamoja na miundo mbinu ya barabara viliwafikia wananchi kwa kiwango cha kuridhisha.

Ukuaji wa uchumi kwa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla waziri Mpango ameliambia bunge kuwa, kiwango cha upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa mwananchi kimepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011-2012 hadi asilimia 26.4 mwaa 2017-2018, huku kina cha umasikini kilipungua kutoka asilimia 6.7 2011-12 hadi asilimia 6.2 mwaka 2017.2018.

Tansania Einwohner von Dar es Salaam, Hassan Kindamba und Hashim Iddy
Wakazi wa Dar es salaam wakifuatilia hotuba ya bajeti kupitia redioPicha: DW/S. Khamis

Wizara ya fedha katika bajeti hiyo inaonesha kuwa mapato ya ndani yameweza kuongezeka kutoka trilioni 18.5 mwaka 2018-2019 kutoka trilioni 11.0 mwaka 2014-15 sawa na ongezeko la asilimia 69.Ukusanywaji wa kodi ikitajwa kuongezeka kwa asilimia 56.5

Aidha waziri mpango amesema katika mwaka wa fedha 2020-2021 watazingatia zaidi kudhibiti matumizi yasio ya lazima, kudhibiti mianya ya rushwa kadhalika kujielekeza katika mukusanyaji wa mapato.

Huko Kenya mambo yakoje?

Waziri wa Fedha nchini Kenya, Ukur Yattani naye aliwasilisha bajeti ya taifa hilo yenye kiasi cha shilingi trilioni 2.7, wakati ambapo taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki likikabiliwa na mdororo wa kiuchumi kutokana na ugonjwa wa covid 19, uvamizi wa nzige pamoja na mafuriko.

 Akizingatia kanuni mpya za kukabiliana na ugonjwa wa covid -19 kwenye bunge lenye wabunge wachache, waziri wa fedha Ukur Yattani, aliwasilisha makadirio ya bajeti yake. Bajeti ya mwaka huu ikizingatia kuchochea uchumi, kubuni nafasi za kazi, viwanda na kuwawezesha vijana. 

Sekta za Elimu, miundo msingi pamoja na usalama zimetengewa fedha nyingi kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021. Hata hivyo viwango vyao vimepunguzwa ikilinganishwa na mwaka uliopita. Majimbo yote 47, yametengewa shilingi bilioni 369. Bunge la Taifa limetengewa shilingi bilioni 37 huku Idara ya Mahakama ikitengewa shilingi bilioni 18. Huku Mamlaka ya Kukusanya Mapato ikishindwa kufikia malengo yake, bejeti ya leo inakabiliwa na nakisi ya karibu shilingi trililioni moja. Waziri wa Fedha ana kibarua cha kujaza shilingi trilioni moja. 

Kenia Wahlwiederholung
Wakazi wa Kibera wakisoma vichwa vya magazetiPicha: Getty Images/AFP/P. Meinhardt

Masaibu ya makamu wa rais William Ruto yaliendelea kushuhudiwa huku baada ya bajeti yake kipunguzwa kwa asilimia 40. Ili kumuepusha Ruto kutumia fedha za mlipa ushuru, wizara ya fedha imepunguza matumizi yake kutoka shilingi bilioni 2.4 hadi 1.4. 
Hata hivyo afisi ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kwa mara ya kwanza imetengewa bajeti ya mwaka mzima kama ya marais watangulizi na makamu wao. Raila ametengewa shilingi milioni 71.9, huku afisi yake ikipokea shilingi milioni 10 kwa mishahara ya wafanyikazi. 

Uganda nayo yaweka wazi matumizi yake

Nchini Uganda pia, waziri wa fedha na uchumi amewasilisha bajeti ya nchi hiyo kwa mwaka ujao wa kifedha. Hata hivyo, baadhi ya watu wameikosoa bajeti hiyo kwa kuzipa kipaumbele sekta za usalama, uchukuzi na barabara badala ya zile za afya na kilimo.

Kwa mujibu wa bajeti hiyo, Uganda inakadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 45, ambapo asilimia 75 zitatokana na makusanyo ya ndani ya nchi. Hii ina maana kuwa raia watatarajiwa kulipa kodi zaidi ili kukidhi bajeti hiyo. Lakini kile ambacho kinawakera wengi ni mgao mkubwa ambao umetolewa kwa sekta ya usalama ikifuata ile ya uchukuzi na barabara. Hata raia wa kawaida wanahisi kilimo na afya vingepewa kipaumbele.

Kwa upande wake rais Museveni ameisifu bajeti hiyo, akitoa angalizo kuwa hata kama uchumi unakadiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia 3.1 badala ya 6 kabla ya janga la COVId-19, ana imani kuwa serikali itakusanya kodi zaidi baada ya yeye kuwafuta kazi wakuu wa Mamlaka ya Mapato URA anaodai walikuwa mafisadi na wazembe. Amesema.