1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali za Afrika zahangaika kuondoa raia wao Ukraine

1 Machi 2022

Visa vya kubaguliwa waaafrika wanaokimbia vita Ukraine vimezifanya serikali za nchi kadhaa za Afrika kuwasaidia wananchi wao kukimbia uvamizi unaofanywa na Urusi

https://p.dw.com/p/47lj5
Ukraine-Krieg | Flüchtlinge aus Afrika und Asien
Picha: WOJTEK RADWANSKI/AFP/Getty Images

Nchi za Kiafrika,Nigeria,Afrika Kusini na nyinginezo ziko kwenye harakati za kuwasaidia raia wao kuondoka Ukraine. Serikali za nchi hizo zinachukua hatua hiyo baada ya kuwepo ripoti za visa vya kibaguzi dhidi ya waafrika katika vituo vya mipaka ya wanakokimbilia.

Visa vya kubaguliwa waaafrika wanaokimbia vita nchini Ukraine vimezifanya serikali za nchi kadhaa za Afrika kuwasaidia wananchi wao kukimbia uvamizi unaofanywa na Urusi nchini Ukraine.

Waafrika nchini Ukraine wengi wao wanafunzi ni miongoni mwa mamia kwa maelfu ya watu wanaojaribu kukimbilia Poland na nchi nyingine jirani na Ukraine. Umoja wa Afrika umezungumzia mashaka yake kuhusu ripoti inayoonesha kuna matukio ya kuwanyanyasa waafrika waliokwama kwenye mgogoro nchini Ukraine,na kusema ni matukio hayo ni ya ubaguzi wa kushtusha.

Ukraine-Krieg | Flüchtlinge aus Afrika und Asien
Picha: ATTILA KISBENEDEK/AFP/Getty Images

Rais wa Senegal ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika Macky Sall pamoja na mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Mouusa Faki Mahamat jana Jumatatu walisema kwamba hasa wametamaushwa na ripoti kwamba wananchi kutoka nchi za Kiafrika walioko upande wa mpaka wa Ukraine wanazuiwa haki ya kuvuka mpaka kukimbilia usalama.

 Taarifa ya pamoja ya viongozi hao imeeleza kwamba ripoti zinazoonyesha waafrika wamebaguliwa na kufanyiwa vitendo visivyostahili zinaonyesha ubaguzi wa kushtusha na ni kinyume na sheria ya kimataifa.

 Aidha taarifa hiyo imekwenda zaidi na kusema nchi zote zinapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa na kuonesha huruma na kuwaunga mkono watu wote wanaokimbia vita bila ya kutazama rangi zao. Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Godfrey Onyeama jana alisema hatua ya kuwaondoa raia wao nchini Ukraine itaanza kesho Jumatano.

Kabla ya hapo mshauri wa rais wa Nigeria,Garba Shehu aliwatolea mwito maafisa wa mpakani wa Ukraine kuwashughulikia raia wa Nigeria kama binadamu mwingine yoyoyte baada ya  ripoti kuonesha kwamba walikuwa wakizuiwa kupanda usafiri wa basi na treni kuelekea mpakani.

Shehu alitowa mfano ulionekana kwenye video moja kwenye mtandao wa kijamii ikimuonesha mwanamke mmoja na mwanawe mchanga akilazimishwa kunyanyuka kwenye kiti kumpisha  mtu mwingine.

Ukraine-Konflik I Grenzkontrollpunkt in Shehyni
Picha: GlobalImagens/imago images

Zimekuwepo pia ripoti za maafisa wa Poland kuwazuia raia wa Nigeria kuingia nchini humo wakitokea Ukraine,na shehu alisema watu wote wanaokimbia vita wana haki sawa ya kutafuta usalama  chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na rangi za hati zao za kusafiri  au rangi ya ngozi zao haziwezi kuwafanya kuwa watu tofauti

Kwa upande mwingine msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini Clayson Monyela ameandika ujumbe wake kwenye mtandao wa Tweeter unaosema kwamba kundi la raia wa nchi yake,wengi wao wanafunzi wamekwama katika vmpaka kati ya Ukraine na Poland.

 Ameendelea kusema kwamba Balozi wa Afrika Kusini mjini Warsaw Poland alikuwa katika eneo hilo kujaribu kuwasaidia kuingia Poland. Kwa mujibu wa Monyela siku ya Jumapili raia wa nchi za Afrika walikuwa wakinyanyaswa katika mpaka wa Poland.

Ingawa  Balozi wa Poland nchini Nigeria Joanna Tarnawska alikanusha madai hayo ya watu kunyanyaswa na kusema kwamba watu wote wanashughulikiwa sawa.Amewaambia waandishi habari ana uthibitisho wa ripoti zinazoonesha tayari baadhi ya raia wa Nigeria wameshavuka na kuingia Poland.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW