1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Uganda yakana kuwatesa wanasiasa na wanahabari

Lubega, Emmanuel4 Septemba 2018

Kufuatia vurugu zilizozuka Uganda katika mji wa Arua. Serikali ya Yoweri Museveni imekanusha vikali madai kwamba maafisa wa vyombo vya usalama waliwatesa na kuwanyanyasa wanasiasa, wanahabari na raia wasio na hatia wakati na baada ya kuwamata washukiwa waliofunguliwa mashtaka ya uhaini.

https://p.dw.com/p/34IEb

Yumkini kikao cha wanahabari kilichoitishwa na mawaziri watatu wa Uganda ambao ni wa usalama, Jenerali Elly Tumwine, Ruth Aceng wa afya na Kaimu Waziri wa Mwongozo wa Kitaifa, Chris Baryomunsi, kililenga kujibu taarifa ndefu aliyosambaza mbunge na msanii Bobi Wine kwenye mitandao ya kijamii akiwa Marekani. 

Katika taarifa hiyo Bobi Wine alisimulia masaibu yake tangu kukamatwa kwake hadi kuachiwa kwenda matibabu Ijumaa iliyopita. Alianza kwa kuelezea kuwa wakati wa kukamatwa alisalimu amri kwa kuinua mikono juu lakini askari anaoelezea kuwa wa kikosi cha ulinzi wa rais, SFC, walimshambulia vibaya na kumsababishia majeraha. Lakini Waziri wa Usalama, Jenerali Elly Tumwine, amekanusha vikali madai hayo akisema kuwa mbunge huyo alijaribu kupigana na maafisa hao. Kwa hiyo walilazimika kutumia nguvu za ziada kumdhibiti na vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwenzake Francis Zake.

Walipata majeraha kwa kushindanana polisi

"Wakati ukiwa unashikwa ukapigana, au ukaanguka chini ukijiumiza mguu au sehemu yoyote, hayo sio mateso, na sheria inasema kama unatisha maisha ya watu wengine unaweza ukapigwa hata risasi," amesema Jenerali Tumwine.

Uganda Sicherheitsminister Gen. Elly Tumwine
Waziri wa Usalama, Jenerali Elly TumwinePicha: DW/E. Lubega

Jenerali Tumwine pamoja na mwenzake wa wizara ya afya, Jane Ruth Aceng, wamesisitiza kuwa wabunge hao wangeweza kupata matibabu nchini, lakini walijifanya kuwa wagonjwa hoi kwa lengo la kushawishi umma kuwahurumia ili kuzidisha madai kuwa haki zao za binadamu zilikuwa zinakiukwa. 

Kuhusu visa vya kuwahujumu wanahabari, ambavyo baadhi vilinaswa kwenye kanda za vidio, waziri wa usalama amelezea kuwa mtu yeyote akiwa katika mazingira ya kikazi anatarajia kukumbwa na hatari husika, hivyo haoni kama kupigwa kwa wanahabari ni jambo la ajabu katika hali za machafuko kama ilivyokuwa. Tamko hilo limezusha hasira miongoni mwa baadhi ya wanahabari.

Hayo yakijiri, kuna madai kuwa taarifa za visa vya machafuko zimeathiri pakubwa sekta ya utalii ya Uganda. Waziri Tumwine amevilaumu baadhi ya vyombo vya habari ndani na nje ya nchi kwa kile alichokidai kusambaza habari hasi zilizozusha hofu na mashaka kuhusu Uganda.

Kwingineko, mahakama kuu imewachia huru watu watano waliokamatwa kuhusiana na mashambulizi ya mabomu mjini Kampala, Julai 2010. Ijapokuwa watu hao wakiwemo Wakenya watatu walikuwa wameachiwa mwaka 2016 baada ya kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha kwamba walihusika, walikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya kupatikana na maandishi ya kuhamasisha ugaidi wakiwa gerezani.