1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Lebanon yaanguka, waandamanaji wadai zaidi

Yusra Buwayhid
30 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Lebanon amejiuzulu Jumanne kufuatia maandamano ya nchini kote ya zaidi ya wiki mbili ya kuipinga serikali. Waandamanaji wamesema hatua hiyo haitoshi. Wanataka mabadiliko ya mfumo mzima wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/3SAdn
Libanon Anti-Regierungsproteste in Beirut
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Hussein

Tangazo la kujiuzulu Hariri kupitia televisheni, lilipokelewa kwa shangwe na waandamanaji ambao wamekuwa wakikusanyika tangu Oktoba 17. Hairri amesema amechukua uamuzi kukidhi matakwa ya raia walio wengi wanaotaka mabadiliko.

Kujizulu kwa Hariri ni ushindi kwa walioandamana, lakini bunge litakabiliwa na kazi kubwa ya kuunda serikali mpya.

Mamia walikusanyika katika mji wa kaskazini wa Tripoli - ngome ya waziri mkuu wa madhehebu ya Sunni - na vile vile mji wa kusini wa Sidoni, inakotokea familia yake.

Waandamanaji wamesisitiza juu ya mabadiliko ya mfumo mzima wa serikali inayotawala kwa mgawanyiko wa kimadhehebu, huku wakisherehekea mwanzo wa utambulisho wa uraia wa kitaifa. Ayman Sharouf ni mmoja wa waandamanaji na anasema bado hawajaridhika. "Kimsingi, tumeshinda sehemu tu ya 'vita', ikiwa tunaweza kusema hivyo. Tunahitaji mabadiliko, tumeanza na serikali, lakini mabadiliko makubwa yatakuwa ya mfumo mzima. Tutabaki kukaa hapa, ili kusema kwamba tunahitaji zaidi ya kile kilichotokea leo, tunahitaji mabadiliko ya mfumo mzima wa Lebanon, " amesema Sharouf.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo aliwatolea wito viongozi wa kisiasa wa Lebanon haraka kuunda serikali mpya. Pompeo amewaambia kuwa maandamano ya amani na umoja wa kitaifa kwa siku 13 zilizopita yametuma ujumbe wazi. Watu wa Lebanon wanataka serikali inayofaa na nzuri, mageuzi ya uchumi, na kukomesha rushwa.

Libanon PK Premierminister Saad al-Hariri in Beirut
Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu Saad al-HaririPicha: Reuters/M. Azakir

Viongozi wa dunia wawatahadharisha wanasiasa Lebanon

Wakati Ufaransa, mmoja wa washirika wa karibu wa Hariri na mshirika muhimu wa Lebanon katika mpango wa msaada wa kiutu wa dola bilioni 11, imeeleza hofu yake ya kwamba kujiuzulu kwa Hariri huenda ikaufanya mgogoro huo kuwa mbaya zaidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon Raya al-Hassan amesema kuondoka kwa Hariri ni muhimu sana ili kulinda utulivu.

Hariri wiki iliyopita alitangaza kifurushi cha mageuzi ya kiuchumi ambayo yanalenga kufufua uchumi ambao umekaribia kuanguka kwa miezi kadhaa sasa, lakini hatua hiyo ilishindwa kumaliza hasira hizo za mitaani.

Viongozi wa kisiasa wa Lebanon wameonekana kushtushwa, wakati huo huo wakijaribu kuwaonyesha huruma waandamanaji wanaodai mabadiliko, pamoja na kuonya dhidi ya misukosuko itakayojitokeza iwapo taifa hilo litakabiliwa na ombwe la kisiasa.

rtre,afp