1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Ujerumani kukuza mahusiano ya kibiashara na Nigeria

30 Oktoba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema analenga kukuza mahusiano ya kibiashara na Nigeria katika sekta ya mafuta na gesi.

https://p.dw.com/p/4YBJN
Nigeria | Bundeskanzler Olaf Scholz trifft Präsident Bola Tinubu
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz (kushoto) akisalimiana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu katika Ikulu ya Abuja: 29.10.2023Picha: Nosa Asemota/Nigeria State House/AP/picture alliance

Scholz ameyasema hayo siku ya Jumapili alipowasili katika mji mkuu wa Nigeria Abuja ambako ameanza ziara yake ya siku tatu huko Afrika Magharibi.

Scholz ambaye anatarajiwa pia kuitembelea Ghana amesema Nigeria ambayo ni nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika ni "soko na mshirika muhimu kwa uchumi wa Ujerumani."

Mwaka jana, kiwango cha biashara kati ya  Ujerumani na Nigeria  kiliongezeka kwa asilimia 50 hadi kufikia dola bilioni 3.2.

Nigeria | Bundeskanzler Olaf Scholz in Abuja
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwasili mjini Abuja, Nigeria: 29.10.2023Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kabla ya kuanzara ziara hiyo, Scholz amesema Ujerumani inatarajia pia kuagiza gesi asilia kutoka Nigeria na kuongeza kwamba wanaangalia mpango wa pamoja wa soko la hidrojeni ambalo ni muhimu kwa siku zijazo.

Kansela Scholz amesisitiza kuwa Ujerumani ina mpango wa kushirikiana na taifa hilo katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, miundombinu, kilimo, teknolojia, rasilimali za madini pamoja na usafirishaji. Kwa sasa Ujerumani inaingiza kiwango kikubwa cha mafuta ghafi kutoka Nigeria lakini si gesi asilia.

Hayo yakijiri, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ataanza Siku ya Jumatatu (30.10.2023) ziara katika mataifa ya Zambia na Tanzania.

Tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na mivutano ya mara kwa mara na China, Ujerumani inalenga kuwa na washirika wapya wa kibiashara hasa katika sekta ya nishati.