1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Kanuni ya ukomo wa deni la taifa kuanza tena 2024

13 Desemba 2023

Serikali ya Muungano ya Ujerumani ya Kansela Olaf Scholz, imefanikisha makubaliano ya bajeti ya mwaka 2024, na kuzuia mzozo wa kisiasa baada ya uamuzi wa mahakama ya kikatiba kutengua makadirio hayo ya mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/4a7L5
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani.
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani.Picha: Liesa Johannssen/REUTERS

Kansela Scholz amesema mipango mipya ya serikali yake itairuhusu Ujerumani kutekeleza ahadi zake za ufadhili kwa Ukraine, pamoja na mipango ya kuvuka hali ya kutoegemea upande wowote kuhusu masuala ya tabia nchi.

Aidha, makubaliano yao yatadumisha ahadi za serikali za ustawi kwa jamii.

"Bajeti ya msingi ya 2024 itatuwezesha kupata karibu euro bilioni 17. Tutafanikisha hili kwa kuondoa ruzuku zinazoharibu hali ya hewa, kupunguza matumizi katika baadhi ya wizara na kupunguza ruzuku za shirikisho." amesema Kansela Scholz.

Ujerumani pia itarejesha kipengele kinachoiruhusu kukiuka ukomo wa deni ambao umewekwa katika sheria za kitaifa kuzuia serikali kukopa zaidi ya asilimia 0.35 ya pato jumla ya taifa kila mwaka.

Mwezi uliopita, mahakama ya juu ya Ujerumani ilibaini kuwa serikali ya Ujerumani ilikiuka sheria ya kikatiba kuhusu deni, kwa kutenga euro bilioni 60 za janga la COVID 19 na kuzihamisha kwenye mfuko wa kushughulikia masuala ya tabia nchi.