1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz ateua Baraza Jipya la Mawaziri Ujerumani

6 Desemba 2021

Olaf Scholz, anayetarajiwa kuchaguliwa na bunge la Ujerumani wiki hii, kuchukua mikoba ya Angela Merkel kuwa Kansela mpya wa taifa hilo, ameteua Baraza Jipya la Mawaziri siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/43u26
Deutschland Regierungsbildung l Koalition von SPD, die Grünen und FDP, in Berlin
Picha: Abdulhamid Hosbas/AA/picture alliance

Katika baraza hilo, usawa wa kijinsia umezingatiwa huku wanawake wakichukua nafasi muhimu katika idara za usalama. 

Scholz, ambaye ni kiongozi wa chama cha Social Democratic SPD ameliteua Baraza lake jipya la mawaziri, kwa serikali ya kwanza itakayoongozwa na chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto baada ya miaka 16 huku mtaalamu wake wa masuala ya majanga Karl Lauterbach akichaguliwa kuwa waziri wa afya.

Soma: FDP yaidhinisha makubaliano ya serikali ya muungano

Lauterbach, aliye na ushawishi na aliyetoa wito wa mara kwa mara wa kuwa na mikakati mikali zaidi ya kupambana na virusi vya corona atakuwa kiongozi muhimu wa serikali kupambana na janga hilo.

Scholz amesema kuwa ana uhakika wajerumani wengi wamemtaka pia Lauterbach kuchukua nafasi hiyo, akiongeza kuwa wahudumu wa afya na madaktari wana haki ya kuona huduma ya afya ikipewa kipaumbele katika sera za Ujerumani.

Karl Lauterbach amechaguliwa kuwa waziri wa afya.
Karl Lauterbach amechaguliwa kuwa waziri wa afya.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Hayo yanajiri wakati vyumba vingi vya wagonjwa mahututi nchini humo vikilemewa na kujaa kupita kiasi wagonjwa wanaugua COVID 19.

Soma: Angela Merkel atajishughulisha na nini baada ya kustaafu?

Scholz anaejieleza kama mtetezi wa haki za wanawake amesema usawa wa kijinsia ni muhimu kwake, ndio maana kati ya mawaziri 16 wanaojumuisha Baraza hilo 8 ni wa kike na 8 ni wa kiume.

Baada ya chama cha kijani ambacho ni mshirika katika serikali ya muungano ijayo nchini Ujerumani kumteua kiongozi mwenza wa chama cha kijani Annalena Baerbock kuwa Waziri wa mambo ya kigeni chama cha SPD kilimchagua Christine Lambrecht, ambaye hadi sasa ni waziri wa sheria atahamia katika Wizara ya Ulinzi.

Kiongozi mwenza wa chama cha kijani Annalena Baerbock amechaguliwa kuwa Waziri wa mambo ya kigeni.
Kiongozi mwenza wa chama cha kijani Annalena Baerbock amechaguliwa kuwa Waziri wa mambo ya kigeni. Picha: Chris Emil Janßen/imago images

Mwanamke mwengine aliyepewa nafasi kubwa katika Baraza hilo la mawaziri ni Nancy Faeser wa SPD atakayekuwa Waziri wa kwanza mwanamke Ujerumani kuiongoza Wizara ya mambo ya ndani, aliyesema kipaumbele chake  cha kwanza ni kushughulikia kitisho kikubwa nchini ambacho ni itikadi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Soma: Merkel aacha urithi wa mchanganyiko Afrika

Kiongozi wa SPD Olaf Scholz aliyeshinda uchaguzi wa Septemba 26, mwezi uliopita alifanikiwa kuwa na makubaliano ya kuunda serikali ya muungano pamoja na chama cha kijani na kile cha FDP.

Chini ya makubaliano hayo vyama hivyo vitatu vimekubaliana kupunguza gesi chafu ya kaboni ikijumuisha kuifanya Ujerumani kutumia kikamilifu nishati endelevu na pia wanalenga kurejea katika kanuni ya ukomo wa serikali kukopa.

Olaf Scholz anatarajiwa kupitishwa rasmi na bunge la Ujerumani siku ya Jumatano kama Kansela mpya wa taifa hilo na rasmi kufikisha mwisho utawala wa Angela Merkel aliyeiongoza Ujerumani kwa miaka 16.