1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia: Visa vya watu kunyongwa vyaongezeka maradufu

22 Julai 2024

Wanaharakati wa haki za binaadamu wamesajili ongezeko la asimilia 42 la visa vya kunyongwa nchini Saudi Arabia katika wakati ambao kuna shinikizo la kufanywa mageuzi kazika taifa hili la kifalme.

https://p.dw.com/p/4ibtk
Wanaharakati wanapinga adhabu ya kunyongwa Saudia
Visa vya kunyongwa watu vimeongezeka karibu maradufu licha ya ahadi za haki za binaadamuPicha: KEVIN DIETSCH/newscom/picture alliance

Wanaharakati wa haki za binadamu wameripoti ongezeko la visa vya kunyongwa nchini Saudi Arabia katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, licha ya ahadi ya utawala nchini humo kuheshimu haki za binadamu. Kufikia Julai 15, serikali iliwanyonga wanaume 98 na wanawake wawili kwa makosa yanayohusiana na mauaji, ugaidi na dawa za kulevya. Hii inaonyesha ongezeko la asilimia 42 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2023. 

Soma pia: Umoja wa Mataifa walaani mauaji Saudia

Ripoti ya shirika la haki za binadamu la Ulaya na Saudia lenye makao makuu yake mjini Berlin, ESOHR, inasema baadhi ya hukumu hizo hazitolewi hata kwa makosa ya kawaida yanayotambuliwa, lakini makosa ya kisiasa kama vile kuhatarisha umoja au usalama wa kijamii.  Waangalizi wa haki za binadamu wamebainisha kwa muda mrefu kwamba aina yoyote ya ukosoaji wa mrithi wa Ufalme, Mohamed bin Salman, au kuunga mkono haki za binadamu unachukuliwa kama ugaidi.

Soma pia: Amnesty: Idadi ya watu walionyongwa iliongezeka mwaka 2022

Mwanamfalme Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al Saud
Mwanamfalme Mohammed Bin Salman anatarajiwa kuwa Mfalme, wakati babake, Mfalme Salman atakapofarikiPicha: Sergei Savostyanov/Sputnik/REUTERS

Ukandamizaji dhidi ya wanaounga mkono haki za binadamu unakinzana kabisaa na dira ya mwaka 2030 ya Saudi Arabia, ambayo ni mradi mkubwa wa marekebisho ya kijamii na kiuchumi nchini humo. Mwanamfalme Mohammed bin Salman alianzisha mageuzi kadhaa mnamo mwaka 2027 katika juhudi za kubadili utegemezi wa taifa hilo kwa nishati ya mafuta, kwa kuwekeza katika teknolojia za kijani, kuimarisha uwekezaji wa nje na kufungua taifa hilo kwa utalii usiyo wa kidini pia kwa kuandaa matukio ya michezo, kama vile michezo ijayo ya Olimpiki ya mtandaoni, au kombe la dunia la kandanda mwaka 2023.

Soma pia: Kesi dhidi ya bin Salman kuhusu mauaji ya Khashoggi yafutwa

Pia, haki za wanawake zimeboreka pakubwa, kwa sababu sasa wanaruhusiwa kuendesha magari, kufanya kazi karibu katika sekta zote na kusafiri peke yao. Hata hivyo hakuna kati ya mageuzi hayo yamehusisha upinzani au miito ya haki za binadamu. Ongezeko la karibuni la vifo vya kunyongwa linakinzana na matamko yaliotolewa na tume ya haki za binadamu ya Saudi Arabia.

Eneo la kutekelezea adhabu ya kifo mjini Riyadh
Matukio ya kunyongwa watu hufanywa hadharani nchini Saudia kwa sababu serikali inaamini yatatumika kuwa mfanoPicha: Johannes Sadek/dpa/picture alliance

Akizungumza na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kujibu mapendekezo ya wajumbe wa baraza hilo kuhusu jinsi ya kuboresha rekodi ya haki za binadamu ya Saudi Arabia kwa kuzingatia haki za msingi, kuzuwia mateso na kufutwa kwa adhabu ya kifo, rais wa tume ya haki za binadamu ya Saudi Arabia Hala bint Mazyad Al-Tuwaijri, alisema Saudi Arabia imedhamiria kusonga mbele kuelekea kufikia viwango bora vya kimataifa katika kulinda na kukuza haki za binadamu, kwa kuzingatia kanuni na maadili yake.

Soma pia: 2015 yavunja rekodi kwa adhabu za vifo zilizotekelezwa

Lakini kwa Ali Adubisi, kiongozi wa shirika la ESOHR lenye makao yake mjini Berlin, maneno hayo ni matupu. "Haki halisi za binadamu zingeweza kuruhusu ukosoaji, ufuatiliaji na uwajibikaji katika mfumo huo wa kimabavu. Ukosefu wa uwajibikaji, pamoja na kuongezeka kwa hukumu za ta'zir kunaweka maisha ya watu 69 hatarini ambao shirika la haki za binadamu linafuatilia kwa sasa. Miongoni mwao kuna watoto 9, 8 kati yao wanakabiliwa na hukumu za ta'zir."

Mnamo mwaka 2023, Saudi Arabia iliwanyonga watu 172, baada ya idadi ya watu 196 mnamo mwaka 2022 ambayo iliongeza idadi ya walionyongwa mwaka 2021 kwa mara tatu na kuongezeka mara saba ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2020. Kichocheo zaidi cha ongezeko hili la mwaka hadi mwaka ni kurejea kwenye adhabu ya kifo kwa makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya. Usitishwaji wa adhabu hiyo ulioanzishwa Januari 2020, ulifikia kikomo Novemba 2022.

Wanawake wa Saudia wanavyozidi kuimarika

Kufikia sasa, kati ya watu 100 walionyongwa mwaka 2024, wafungwa 66 walikabiliwa na mashtaka ya mauaji, huku adhabu 34 zilizosalia zikiathiri watu ambao walishtakiwa kwa ugaidi na dawa za kulevya. Kuongezeka kwa mauaji kumebainishwa zaidi na kuongezeka kwa matumizi ya hukumu za 'ta'zir'. Hukumu ambazo msingi wake ni ta'zir ni za kiholela kwani adhabu hiyo haifafanuliwi na tafsiri ya Saudi Arabia ya sheria za Kiislamu - inayojulikana zaidi kama Sharia - lakini na majaji binafsi.

Kulingana na ESOHR, upo uwezekano kwamba kwamba ta'zir imetumika kwa kiwango kikubwa kutokana na ukosefu wa uwazi kuhusu mahakama hizo na aina za hukumu katika taarifa mbalimbali zinazohusiana na hukumu ya kifo zinazotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia.

Mwandishi: Jennifer Holleis/DW Mashariki ya Kati

Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Bruce Amani