1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia na gharama za ukiukaji haki za binadamu

Josephat Charo
3 Septemba 2020

Je, Saudi Arabia inaweza kumudu gharama za ukiukaji wa haki za binadamu? Saudi Arabia imekuwa ikikata mawasiliano kati ya wakosoaji walio magerezani na familia zao.

https://p.dw.com/p/3hwCN
USA Washington | Mohammed bin Salmad während Treffen mit Jim Mattis im Pentagon
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Mrithi mwanamfalme Mohammed bin Salman huenda akalipa gharama kutokana na hali hiyo, iwapo itasababisha msuguano katika mahusiano na washirika wa kimataifa. 

Maafisa wa Saudia wamekuwa wakiongeza ukandamizaji dhidi ya wakosoaji, ikimtia mbaroni jamaa wa familia ya mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi, Saad Aljabri, wiki hii na kukata mawasiliano kati ya wakosoaji wanaotumikia vifungo magerezani na familia zao. Hayo yamesemwa na familia hizo.

Maafisa tayari wamewakamata watoto wawili wa Aljabri na kaka yake mnamo mwezi Machi kabla ya kukata rufaa mwezi huu nchini Marekani, akidai kwamba mrithi mwanamfalme wa Saudia alijaribu kumuua.

Mtoto wake mwingine wa kiume, Khalid, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twita siku ya Jumatano kwamba ukamataji wa hivi karibuni wa shemeji wa Aljabri ni jitihada ya wazi ya kuihangaisha familia yake.

Wakosoaji wengine wengi wanaotumikia vifungo gerezani wamepunguziwa idadi ya simu wanazotakiwa kupiga mara kwa mara au safari za kutembelewa na jamaa wa familia zao kukatizwa katika miezi ya hivi karibuni.

Saudische Frauenrechtlerin Loujain al-Hathloul
Mwanaharakati wa Saudia Loujain al-Hathloul Picha: Reuters/ Amnesty International/M. Wijntjes

Lina al-Hathloul, dada yake Loujain al-Hathloul, mwanahrakati mashuhuri wa haki za binadamu, alisema familia yake ina wasiwasi mkubwa sana kwamba haijasikia chochote kutoka kwa Loujain tangu tarehe 9 mwezi Juni mwaka huu. Akizungumza na DW, Lina amesema mara ya kwanza dada yake alipozuiliwa bila kufunguliwa mashitaka, alikuwa anateswa kwa hiyo hawezi kufikiria kitu kingine chochote anachofanyiwa sasa dada yake.

Ukandamizaji huu unakuja wakati hali ikiwa tete katika mahusiano kati ya Saudi Arabia na washirika wake. Wataalamu wamegawanyika kuhusu ikiwa mrithi mwanamfalme Mohammed bin Salman yuko tayari kwa athari zitakazojitokeza na ikiwa ataweza kulipa gharama kutokana na msuguano utakaojitokeza. Kuendelea kuwakaba koo wakosoaji yumkini kukayavuruga mahusiano ya Saudia na Marekani. Akiwa katika kampeni mwaka uliopita, mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden, aliitaja Saudia kuwa taifa lisilopendwa kutokana na ukandamizaji wake na kutishia kusitisha kuuzia silaha ufalme huo. Msuguano huenda ukauimarisha msimamo wake Biden, ambao huenda ukaleta tofauti iwapo atashinda uchaguzi wa rais mwezi Novemba.

Maseneta wanne wa Marekani wamemshinikiza rais Donald Trump asaidie kuhakikisha familia ya Aljabri, ambaye aliisaidia idara ya ujasusi ya Marekani kwa miaka kadhaa, iachiwe huru. Makundi ya washawishi pia yamejitokeza kuongeza shinikizo la kuachiwa huru mwanamfalme Salman bin Abdulaziz bin Salman al Saud mwezi Mei.

Jamal Khashoggi
Jamal Khashoggi, mwandishi wa Saudia aliyeuawa kinyamaPicha: picture-alliance/newscom/AFP/Getty ImagesTNS

Kisima cha ari ya kisiasa kimeanza kukauka. Barani Ulaya, uamuzi wa Ujerumani kuhusu ikiwa irefushe marufuku ya uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia kabla kufika mwisho mwezi Desemba, inaipa fursa ya kuishinikiza kuhusu suala la haki za binadamu. Ujerumani ilisitisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia kufuatia mauaji ya mkosoaji mwandishi habari Jamal Khashoggi mnamo mwaka 2018, uhalifu ambao umehusishwa na mrithi mwanamfalme, Mohammed bin Salman, pamoja na kuwatupa gerezani wanaharakati, mambo ambayo yaliitia doa sifa yake kama mwanamageuzi na kuvuruga mahusiano na wawekezaji wa kimataifa.

Huku Saudia ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kundi la nchi tajiri na zile zinazoinukia kwa kasi duniani G20, mwezi Novemba, mrithi mwanamfalme Mohammed bin Salman ana fursa nzuri kurejesha sifa na heshima yake. Lakini wakati bunge la Ulaya litakapokutana baada ya kupindi cha mapumziko cha msimu wa joto, wabunge watataka hatua ichukuliwe kuhusu maombi ya muda mrefu ya kutaka binti wa kifalme Basmah bint Saud na mwanamfalme Salman bin Abdulaziz waachiwe.

Wataalamu wanaonya kwamba ongezeko la kasi ya uuzaji silaha kwa Saudi Arabia katika muongo uliopita ni ishara kwamba mashirikiano ya kimataifa katika suala la usalama wa kikanda yanakwamisha kesi moja moja za ukiukaji wa haki za binadamu.