1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bin Salman ajitwika jukumu mauaji ya Khashoggi

30 Septemba 2019

Mrithi wa kiti cha ufalme nchini Saudia Arabia Mwanamfalme Mohammed bin Salman amesema wakati mahojiano na televisheni moja ya Marekani kuwa anabeba jukumu la mauaji ya kikatili ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/3QTgY
Mohammed bin Salman Kronprinz Saudi Arabien
Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi ArabiaPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Wakati wa mahojiano hayo na kituo cha televesheni cha CBS yaliyorushwa jana Jumapili, Bin Salman ameyataja mauaji ya Jamal Khashoggi kuwa uhalifu wa kiwango kibaya kabisa na anajitwika dhamana ya mkasa huo kwa sababu ulifanywa na watumishi wa serikali ya Saudi Arabia.

Alipoulizwa iwapo aliamuru kutekelezwa mauaji hayo Bin Salman alijibu ´hapana´ na kurejea kusema kwa mara nyingine kuwa tukio hilo lilikuwa kosa kubwa.

Bin Salman ameahidi kuchukua hatua zote kuzuia kisa kama hicho kutokea katika siku zijazo

Khashoggi, mwandishi habari na mkosoaji mkubwa wa ufalme wa Saudia Arabia aliingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Instabul, Uturuki mnamo Oktoba 2, 2018 kwa lengo la kuchukua nyaraka kumwezesha kufunga ndoa na mchumba wake raia wa Uturuki.

Maafisa wa serikali ya Saudi Arabia walimuua mwandishi huyo ndani ya ubalozi huo na kisha kuukata kata mwili wake  ambao hadi leo haujapatikana.

Hakuna aliyetiwa hatiani kutokana na mkasa huo

Bahrain | Journalist Jamal Khashoggi
Mwandishi Habari, Jamal KhashoggiPicha: picture-alliance/dpa/Bildfunk/H. Jamali

Saudi Arabia imewafungulia mashtaka watu 11 kuhusiana na kisa hicho lakini kesi dhidi yao zinaendeshwa kwa siri na hadi sasa hakuna mtu aliyetiwa hatiani kutokana na kifo cha Khashoggi.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema Saudia Arabia inabeba jukumu la mauaji ya Khashoggi na kuongeza lakini wajibu wa mwanamfalme Salman katika kisa hicho unapaswa kuchunguzwa.

Mjini Washington, Bunge la Marekani limesema linaamini Bin Salman anahusika moja kwa moja na mauaji ya Khashoggi.

Lakini Saudi Arabia imesisitiza mwanamfalme huyo hakuhusika kwa njia yoyote katika operesheni ya kumuua Khashoggi iliyotekelezwa na maafisa wa serikali wanaowajibika moja kwa moja kwa Bin Salman.

Maswali ni mengi kuliko majibu

Großbritannien l Proteste gegen Saudi-Arabien im Fall Khashoggi in London
Picha: Getty Images/J. Taylor

Alhamisi iliyopita, mchumba wa Kashoggi Hatice Cengiz alisema mauaji ya mwandishi huyo bado yameacha maswali mengi na kumtaka mwanamfalme Salman kumpa majibu juu ya kwanini Khashoggi aliuwawa, mwili wake uko wapi na ipi ilikuwa sababu ya kuuliwa kwake.

Maswali kama hayo yameulizwa pia na rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan ambaye amesisitiza kuwa nchi yake

itaendelea kutafuta ukweli juu ya mauaji ya Khasshoggi akisema baadhi ya wale waliohusika wanaukwepa mkono wa sheria.

Katika makala iliyochapishwa na gazeti la Washington Post, Erdogan amesema Uturuki bado inahitaji kufahamu yalipo mabaki ya mwili wa Khashoggi na nani aliamuru kutekelezwa kwa operesheni ya mauaji yake.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa japo Uturuki inaizingatia Saudi Arabia kuwa nchi rafiki na mshirika wa kutumainiwa, lakini hilo halimaanishi kuwa serikali mjini Ankara itafunga mdomo juu ya suala la Kashoggi.