1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia kikaangoni juu ya rekodi ya haki za binadamu

Sylvia Mwehozi
5 Novemba 2018

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinakutana mjini Geneva Jumatatu kupitia rekodi ya haki za binadamu ya Saudi Arabia mnamo wakati taifa hilo likikabiliwa na shutuma juu ya mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi. 

https://p.dw.com/p/37eiG
Portraitfoto: Mohammed bin Salman
Picha: picture-alliance/AP/A. Nabil

Mjadala huo wa umma wa nusu siku mbele ya baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu, unakuja mwezi mmoja baada ya mkosoaji wa ufalme wa Saudi Arabia kuuawa katika ubalozi mdogo mjini Istanbul.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Uturuki alithibitisha kwa mara ya kwanza wiki iliyopita kwamba Khashoggi, aliuawa mara alipoingia katika ubalozi mnamo Oktoba 2 ikiwa ni sehemu ya mpango wa kumuua, kisha mwili wake ulikatwakatwa na kuharibiwa.

Mauaji hayo yameupaka doa uhusiano wa Saudi Arabia na Marekani pamoja na mataifa mengine ya magharibi na kuleta taswira mbaya kuhusu mrithi wa kiti cha ufalme Mohammed bin salman.

Türkei Istanbul | Protest gegen Mord an Jamal Khashoggi vor Konsulat Saudi-Arabiens
Waandamanaji wakiwa wamebeba picha ya mwandishi Jamal KhashoggiPicha: picture-alliance/abaca/Depo Photos

Kikao cha leo ambacho huzikutanisha nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kila baada ya miaka minne, pia kitaangazoa wajibu wa Saudi Arabia kwenye vita vya Yemen.

Saudi Arabia na washirika wake waliingilia kijeshi vita vya Yemen mwaka 2015 ili kumuunga mkono rais Abedrabbo Mansour Hadi, baada ya waasi wanaoungwa mkono na Iran kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, watu wapatao 10,000 wameuawa katika mgogoro huo na jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamezituhumu pande zote za waasi wa Kihouthi na muungano wa kijeshi ukiongozwa na Saudi Arabia kwa vitendo vinavyoweza kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita. Mgogoro huo pia umetengeneza mzozo mkubwa wa kiutu duniani na kuwaacha mamilioni ya watu wakiwa katika baa la njaa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Marekani ambayo kwa muda mrefu imeunga mkono muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, wiki iliyopita ilitoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi ya anga ya muungano huo katika taifa la Yemen.

Jemen | Humanitäre Krise
Mtoto aliyeathirika na vita ya YemenPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/H. Mohammed

Ujumbe wa Saudi Arabia mjini Geneva hii leo, utaongozwa na Bandar Al Aiban ambaye ni mkuu wa tume ya haki za binadamu ya nchi hiyo. Ujumbe huo utawasilisha ripoti ya namna nchi hiyo inavyojitahidi kuheshimu haki za binadamu za kimataifa na pia watajibu maswali na maoni kutoka nchi wanachama wa umoja huo kuhusiana na rekodi yao.

Baadhi ya nchi tayari zimewasilisha orodha ya maswali kwa ajili ya kikao cha mapitio ikiwemo maswali ya moja kwa moja kutoka Uingereza, Austria na Switzerland juu ya kesi ya mauaji ya Khashoggi.

Saudi Arabia tayari ina rekodi ya kuendelea kutumia adhabu ya kifo na ongezeko la adhabu ya kunyongwa pamoja na matumizi ya sheria ya kupambana na ugaidi ambayo inalalamikiwa kwamba inatumika vibaya.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Caro Robi