1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sasa Cote d'Ivoire yatumbukia shimoni

12 Januari 2011

Hali inazorota Cote d'Ivoire na sasa dalili za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe zimeanza, licha ya jitihada za viongozi wa ECOWAS na AU kuumaliza mgogoro kati ya Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara kwa njia za amani.

https://p.dw.com/p/zwaw
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Iviore
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'IviorePicha: AP

Asubuhi ya leo askari mmoja ameuawa, baada ya vikosi vitiifu kwa Laurent Gbagbo kuvamia makaazi ya wafuasi wa Alassane Ouattara katika mji wa Abobo. Kwa mujibu wa mashahidi, miripuko, kutoka kile kinachoaminiwa kuwa ni silaha nzito, imesikika katika eneo hilo, kuanzia usiku wa manane.

"Sijapata kusikia mshindo mzito wa silaha kama ule. Nikiwa ndani ya nyumba yangu, niliona muili mmoja wa askari polisi." Abdoulaye Cisse, ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio, ameliambia Shirika la Habari la Reuters.

Mapambano ya silaha katika eneo hili hili hapo jana, yaliua watu watano, watatu kati yao wakiwa maafisa wa usalama kutoka vikosi vinavyomtii Gbagbo.

Mauaji, Utekaji Nyara na Wakimbizi

Balozi wa Cote d'Iviore kwenye Umoja wa Mataifa, Youssoufou Bamba, ambaye anawakilisha serikali ya Alassane Ouattara.
Balozi wa Cote d'Iviore kwenye Umoja wa Mataifa, Youssoufou Bamba, ambaye anawakilisha serikali ya Alassane Ouattara.Picha: picture alliance/dpa

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, vurugu zilizoanza tangu upigaji kura hapo Novemba 28, mwaka jana, zimeshagharimu maisha ya watu 200; mamia kutekwa nyara na huku wengine 20,000 wakiripotiwa kuyakimbia makaazi yao na kukimbilia katika nchi jirani ya Liberia.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba wengi kati ya waliouawa au kutekwa nyara ni kutokana na kumuunga mkono kwao Ouattara, na kwamba vitendo hivyo hufanywa na vikosi vya Gbagbo wakishirikiana na makundi ya wanamgambo katika nyakati za usiku.

Hata hivyo, upande wa Gbagbo unakana madai haya, ukisema kwamba kuna polisi wengi ambao wameuawa na wanaharakati wanaomuunga mkono Ouattara.

Machafuko haya ya sasa yanaonekana ni dalili za karibuni zaidi za nchi hiyo ya Magharibi ya Afrika kutumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo limekuwa likiepukwa na wasuluhishi wa ECOWAS na AU, ambao wanamtaka Gbagbo aondoke madarakani kwa hiari yake, kabla nguvu ya kijeshi haijatumika.

Gbagbo king'ang'anizi

Laurent Gbagbo: "Siondoki madarakani ng'o!"
Laurent Gbagbo: "Siondoki madarakani ng'o!"Picha: picture alliance / dpa

Lakini Gbagbo ameshasema wazi kwamba, kuondoka madarakani si jambo linalokubalika na kwamba hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya utawala wake, italiingiza eneo zima la Magharibi ya Afrika kwenye matatizo.

Cote d'Ivoire inapakana na Ghana na Liberia, ambapo tayari Ghana imeshakataa matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Gbagbo kwa kuhofia wimbi la wakimbizi wa Cote d'Iviore kuingia ndani ya mipaka yake, huku Liberia ikiwa tayari imeshaanza kupokea maelfu ya wakimbizi.

Cote d'Ivoire imepasuka karibuni katikati baina ya Kusini na Kaskazini, na mvutano wa Gbagbo na Ouattara ni kielelezo tu cha mpasuko huo, ambapo Kusini kwenye Wakristo wengi kunamuunga mkono Gbagbo na Kaskazini kwenye Waislam wengi kunamuunga mkono Ouattara.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman