1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanders kuchuana tena na Biden katika majimbo sita

Sylvia Mwehozi
10 Machi 2020

Wapiga kura jimboni Michigan na majimbo mengine matano wanapiga kura Jumanne katika kura za mchujo zitakazoamua ikiwa ni Joe Biden ama Bernie Sanders atakayepambana na rais Donald Trump kwenye uchagzi wa mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/3ZA4r
Iowa, Des Moines: CNN - Präsidentschaftskandidaten der Demokraten
Picha: Getty Images/R. Beck

Majimbo ya Idaho, Mississippi, Missouri, North Dakota na Washington yaliyo na jumla ya wajumbe 352 pia yanapiga kura hii leo. Lakini Michigan ambalo lina wajumbe wengi karibu 125, linatazamwa na wagombea wote wawili ili kuibuka na ushindi. Sanders anahitahi kupata ushindi jimboni Michigan, ili aweze kubaki kama mgombea anayefaa.

"Tutafanya kila linalowezekana kuondoa aina yoyote ya ubaguzi katika nchi hii. Tumechoshwa na mfumo wa kibaguzi ndani ya Marekani. Tumechoka na pengo kubwa ambapo familia za weupe zina utajiri mara kumi ya familia nyeusi. Tumechoka na vifo vya akimama weusi kuliko akinamama weupe. Tumechoka na mfumo wa afya ambao hautoi haki kwa jamii ya wamarekani weusi," alisema Sanders.

USA Super Tuesday | Bernie Sanders und Joe Biden ARCHIV
Wagombea wawili waliobaki kuchuana kura za mchujo za DemocraticPicha: picture-alliance/dpa/M. Rourke

Wanasiasa wote wawili mmoja akielemea mrengo wa kati na mwingine mrengo wa kushoto, wamesalia katika ushindani mkubwa wa kuteuliwa na chama cha Democratic, wakati wagombea wengine wakijiondoa na wengi kumuunga mkono Biden. Sanders ambaye mwanzoni mwa mwaka alikuwa ni mgombea anayeongoza na kufanya vyema kwenye majimbo matatu ya mwanzo, ghafla aliwekwa nafasi ya pili baada ya Biden kujizolea ushindi katika jimbo la South Carolina na kisha kushinda majimbo 10 kati ya 14 katika Jumanne muhimu.

Biden naye amewaeleza wapiga kura kwamba ataiunganisha tena Marekani.  "Tutafanya hivi kwa kuleta umoja Marekani, kuwaunganisha Wamarekani wa kila kabila, kila jinsia, kila rangi na kila hali ya kiuchumi. tutawaunganisha Wademocrats, Warepublican na kila mtu binafsi. Hicho ndicho tunachohitaji kama taifa, tutainganisha nchi."

Biden mwenye umri wa miaka 77 amejipatia uungwaji mkono na wagombea kadhaa waliokuwepo awali kwenye kinyang'anyiro cha uteuzi ndani ya Democratic, wakiwemo maseneta wawili muhimu weusi. Maseneta hao ni Cory Booker wa New jersey ambaye alitangaza kumuunga mkono Biden siku ya Jumatatu na Kamala Harris wa jimbo la California. Wabunge wote wawili wanatajwa kwenye uteuzi wa nafasi ya makamu wa rais ikiwa Biden atapita. Wagombea wengine wa zamani katika kinyang'anyiro hicho Pete Buttgieg, Amy Klobuchar, Michael Bloomberg na Reto O'Rourke wote walitangaza kumuunga mkono Biden. Biden alihudumu miaka nane kama makamu wa rais chini ya utawala wa Barack Obama.