1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanders atangaza ushindi New Hampshire; Biden aanguka tena

Sekione Kitojo
12 Februari 2020

Mwanasiasa  Bernie Sanders ametangaza  ushindi  katika  kura  ya mchujo kwa chama cha  Democratic katika jimbo la New Hampshire, akipata ushindi mwembamba mbele  ya mgombea anayemfuata Pete Buttigieg,meya wa zamani.

https://p.dw.com/p/3Xdtq
Vorwahlen in den USA - New Hampshire Bernie Sanders
Picha: Reuters/R. Wilking

Bernie Sanders , ambaye  ni  Seneta  wa  chama  cha  Democratic , ametokea  wa  kwanza  akiwa  na  kiasi  ya  asilimia  26  ya  kura, akifuatiwa  na  Pete Buttigieg, ambaye  amepata  kiasi  ya  asilimia 24, wakati  ambapo  zaidi  ya  asilimia  90  ya  kura  zimehesabiwa, kwa mujibu  wa  vyombo  vya  habari  nchini  Marekani ikiwa  ni pamoja  na  CNN. Katika  hotuba  yake  ya  ushindi  kwa  wafuasi wake  Bernie Sanders  amesema  huu  ni  mwanzo  wa  mwisho  wa Donald Trump.

USA Buttigieg und Sanders bei TV-Debatte der US-Demokraten unter Beschuss
Bernie Sanders mfuasi wa siasa za mrengo wa kushoto, ameshinda New HampshirePicha: AFP/Timothy A. Clary

"Sababu  ambayo  imetufanya  tushinde leo hapa New Hampshire, tumeshinda  wiki  iliyopita  Iowa, kwa sababu  ya  kazi  kubwa iliyofanywa  na  watu  wa  kujitolea. Na nataka  kuwaambia leo, kwamba  ushindi  huu  hapa  ndio  mwanzo wa  mwisho  wa  Donald Trump."

"Haijalishi  nani  anashinda, na  kwa  hakika  tunatumai itakuwa  sisi, tutakuwa   pamoja  na  kumshinda  rais hatari kabisa  katika  historia ya  hivi  sasa  katika  nchi  hii," sanders  alisema. Wagombea wamekuwa  wakitoa  ujumbe  wa  umoja  katika  chama. Katika nafasi  ya  tatu  bila  kutarajiwa  alikuwa  Amy Klobuchar , akiwa  na karibu asilimia  20  ya  kura, ambaye  anajaribu  kuelekea  katika nafasi  ya  juu  kwa  ujumbe  ambao si rahisi  lakini  wenye matumaini. Elizabeth Warren  na  aliyekuwa makamu wa rais  Joe Biden  wametupwa  nyuma  wakiwa  na  asilimia  9  na  8 ya  kura.

Vorwahlen in den USA - New Hampshire Joe Biden
Joe Biden ametupwa mbali akitokea wa tano katika kura ya mchujo jimboni New HampshirePicha: picture-alliance/AP Photo/M. Kinnard

Mbio  hizo za  kuwania  kuteuliwa  sasa  zinaelekea  katika  jimbo  la Nevada na  South Carolina, majimbo  ambayo  yana  wakaazi  zaidi wa  Kilatino  na  Wamarekani  wenye  asili  ya  Afrika,  tofauti  na jimbo  lenye wazungu  wengi  la  New Hampshire.

Uchaguzi  katika  eneo  la  kaskazini  mashariki , uchaguzi  halisi  wa kwanza  wa  mchujo  katika  mzunguko  huo , unafuatia  mjadala jimboni Iowa  katika  eneo  la  kati  magharibi, ambako  matokeo  ya kura  za  mchujo  yalivurugika  na  hadi  leo yanabishaniwa.  Buttigieg na  Sanders  wanaongoza  Iowa, na  wamekuwa  watu  wa  mbele kwa  sasa.

Vorwahlen in den USA - New Hampshire Pete Buttigieg Anhänger
Wafuasi wa Buttigieg wakishangiriaPicha: Reuters/E. Thayer

Biden , ambaye  alionekana  kuwa  ni  mgombea  anayeongoza, amekuwa  wa  nne  katika  matokeo  ya  awali  ya  Iowa na aliondoka  New Hampshire  kabla  ya  matokeo  kutolewa, akipendelea  kuelekea  South Carolina  ambako  ana  uungwaji mkono  miongoni  mwa  wapiga  kura  Wamarekani  weusi.