1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia, "Tanzania haigawiki, wala haiuziki"

13 Juni 2023

Kumekuwa na maoni mchanganyiko nchini Tanzania baada ya rais Samia Suluhu Hassan kuzungumzia kwa mara ya kwanza sakata la mkataba wa uendeshaji wa bandari akisema "Tanzania haiwezi kugawanyika wala kuuzwa."

https://p.dw.com/p/4SVlg
Tansania Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Presidential Press Service Tanzania

Kauli ya Rais Samia aliyeitoa wakati akizungumza na wananchi jijini Mwanza inakuja huku mjadala kuhusu sakata la bandari zilizoko nchini kupewa kwa kampuni moja ya kigeni ukizidi kushika kasi na wachambuzi wa mambo wanasema kiongozi huyo wa nchi ametumia turufu yake kutuliza hali ya mambo.

Ikiwa ni kauli yake ya kwanza kuhusiana na kile kinachoendelea kujadiliwa, Rais Samia alitumia maneno mafupi kuonyesha namna utawala wake ulivyo dhabiti kushughulikia maendeleo ya wananchi akisisitiza kwamba Tanzania haiwezi kugawanywa.

"Na Tanzania ni moja.. haigawanyiki wala haiuziki. Kwa hiyo ndugu zangu... mama ni mTanzania... maendeleo ni muhimu," alisema rais Samia.

Hatua hiyo imepokelewa kwa hisia mseto kutoka kwa makundi mbalimbali ya wachambuzi wa mambo pamoja na wananchi, huku baadhi wakisema Rais Samia amejitokeza wakati muafaka wakati mjadala kuhusu suala hilo ukiendelea kutikisa kila kona ikiwemo mijadala inayosema  taifa hili huenda likawekwa rehani kwa wawekezaji wa kigeni.

Treni ya mizigo inayosafirisha kontena iliyosheheni bidhaa kutoka Uingereza, ikijiandaa kuondoka kutoka kituo cha reli kinachoendeshwa na DP World London. Kampuni hii imekuwa ikiendesha idara za bandari kwenye mataifa mbalimbali duniani.
Picha: Getty Images/AFP/I. Infantes

Mmoja wa wachambuzi wanayofuatilia kwa karibu yale yanayoendelea kwa wakati huu, Eric Benard anasema kauli ya Rais Samia ni ujumbe wenye lengo la kuwaangazia wale wanaojaribu kukosoa sera zake za kuwakaribisha wawekezaji wa nje. Alisema "Kwa hiyo ni ujumbe pia kwa wale mahasimu wake wa kisiasa.. ni ujumbe pia kwa jamii ya kimataifa.. ni ujumbe pia kwa wale wote wenye nia tofauti na yeye..."

Licha ya serikali kujitokeza mara kwa mara kujaribu kuweka sawa kuhusiana na mkataba huo, bado wasiwasi unaendelea kusalia kwa wananchi wengi na huku baadhi ya wachambuzi wanaongeza kwa kusema kauli ya Rais Samia inadhihirisha namna suala hilo la mikataba ya kigeni linavyoendelea kuwa gumu na tete.

Soma Zaidi: Ukodishaji wa bandari ya Dar es Salaam waibua mjadala

Bado makundi mbalimbali ya wasomi na wanasiasa wanaendelea kujitokeza hadharani kukosoa mazingira ya mkataba kati ya serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai iliyopewa mamlaka kupitia kampuni yake ya DP World kuendesha shughuli zote za bandari nchini.

Viongozi wa dini pia jana walionya vikali juu ya hatua hiyo wakitaka kutupiwa macho baadhi ya maeneo yanayotajwa kuwa na utata.

Sikiliza Zaidi: 

Upi msimamo wa serikali juu ya uendeshaji wa bandari?