1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia: "Naendeleza kazi ya mtangulizi wangu"

Admin.WagnerD19 Aprili 2021

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameonya amewaonya watu wanaomtofautisha na mtangulizi wake hayati John Magufuli na kuuema anaiendeleza kazi iliyoanzishwa na kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/3sDEa
Samia Suluhu, Vizepräsidentin Tansania
Picha: DW/Said Khamis

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameonya dhidi ya watu na wanasiasa wanaomtofautisha na mtangulizi wake hayati John Magufuli akisisitiza kuwa serikali yake inaenzi na kuendeleza kazi zilizofanywa na kiongozi huyo aliyeaga dunia mwezi uliopita. Matamshi ya rais Samia aliyoyatoa jana wakati akihutubia kongamano la kidini lililofanyika jana mjini Dodoma yanakuja wakati wafuatiliaji wa siasa za nchi wanasema utendaji wake unaonesha tofauti na mtangulizi wake.

Soma Zaidi: Mfahamu Rais ajaye wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suhulu Hassani amewakumbusha wabunge wa chama chake kwamba serikali ya sasa ni mwendelezo wa mambo yaliyoanza kutekelezwa tangu wakati wa awamu ya tano ya uongozi na yeye akiwa namba mbili ya utawala huo.

Ingawa Rais Samia Suluhu Hassani ametengua kitendawili cha mvutano uliokuwa bungeni baina ya wabunge hao wa CCM chama kinachoongoza dola, lakini katika uwanda wa kisiasa na sera, huenda Rais Samia amejipambanua kivingine na mtangulizi wake, Hayati Rais Magufuli.

Tansania Dodoma | Wahlkampf | CCM Partei
Picha: DW/S. Khamis

Hatua yake ya kutaka kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari, ufufuaji na uimarishaji wa mahusiano na mataifa ya kigeni, kuepuka matumizi ya nguvu nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya taifa na mpaka eneo la ushughulikiaji wa janga la virusi vya corona, ni baadhi ya mambo ambayo yanaweka alama ya tofauti baina ya viongozi hao wawili.

Utawala uliopita kwa sehemu fulani uliyapa kisogo masuala hayo na wakati huu yanaonekana kupewa umuhimu wa pekee.

Bila shaka wawili hao wanaweza kuwa ni watu wamoja yaani kitu kimoja katika masuala ya utekelezaji wa ilani ya chama kinachoendelea kuikalia dola,lakini haiba yao ni jambo lingine linalowatofautisha kwa kiwango kikubwa.

Huenda pia, Rais Samia Suluhu Hassani ametaka kuwatumia ujumbe wabunge wa chama chake kuwa hawapaswi kufarakana hasa wakati huu kukiwa na bunge linalotawaliwa na chama kimoja.

Ingawa bado ni vigumu kupima moja kwa moja ni upande upi wa wabunge utajihesabu kushinda kati ya wale waliokuwa wakikosoa rekodi ya utawala wa Magufuli na waliokuwa wakiutetea na kuupongeza, hata hivyo CCM itapaswa kuchukua hatua za kujitafakari hasa wakati huu kinapoelekea katika mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti mpya ambaye atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

George Njogopa