1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SADC yazindua kituo cha kupambana na ugaidi

28 Februari 2022

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika Sadc leo zimezindua kituo cha kukabiliana na ugaidi huku wimbi hilo la uhalifu huo likionekana kuota mizizi katika baadhi ya nchi wanachama.

https://p.dw.com/p/47jOp
Mosambik | Besuch Filipe Nyusi und Paul Kagame in der Provinz Cabo Delgado
Picha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Kituo hicho kilichozunduliwa jijini Dar es salaam ni sehemu ya mkakati wa jumuiya hiyo kukabiliana na tishio la matukio ya kigaidi hasa wakati ambako mataifa kama Msumbiji na Eswatini yakiendelea kuandamwa na matukio ya kigaidi.

Nchi wanachama zinaamini kuwa kituo hicho kitakuwa kiini cha kukusanya na kuchakata taarifa za kiintelijensia ambazo zitasaidia kuzibaini njia watumiazo wenye makundi ya kigaidi.

Uzinduzi huo ambao mchakato wake ulianzishwa tangu mwaka 2019 unakuja katika wakati ambapo mataifa kama Afrika Kusin na Malawi yakilazimika kuongeza idadi ya askari kwenda kukabiliana na wapiganaji wa kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.

Präsident von Mosambik besucht Militärstützpunkt
Mkoa wa Cabo Delgado unakumbwa na ugaidiPicha: Roberto Paquete/DW

Kulingana na Waziri wa ulinzi wa Tanzania, Stergomena Taxi, nchi wanachama zinatambua namna ugaidi unavyoendelea kuwa tishio la usalama duniani kote, hivyo kuanzishwa kwa kituo hicho kumekuja katika wakati muafaka.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusin, Candith Mashego-Dlamini amesema ni mihimu kwa nchi za kanda hii kuendelea kuimarisha ushirikiiano  ili kushinda vita dhidi ya vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya nchi wanachama wake. Nchini Msumbiji tuna vikosi vya Sadc viko huko… Jeshi la Afrika Kusini limetumwa huko, kadhalika jeshi Malawi pia ili kuisaidia Msumbiji kukabiliana na magaidi wanaangamizi watu wa msumbiji.

 Afrika ni kati ya maeneo ambayo vitendo vya kigaidi vinaonekana kuendelea kuongezeka na kuzidisha wasiwasi juu ya majaliwa ya bara hili kwa siku za usoni.

Ripoti iliyotolewa na shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2007 hadi 2016 afrika ilipoteza kiasi cha dola za Marekani bilioni 119 katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, kiasi cha fedha ambazo kinaelezwa kuwa kingeweza kutumika katika shughuli nyingine za uharakishaji maendeleo.

George Njogopa/DW Dar es Salaam