1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yawakamata watu 66 kwa kubeza mauaji ya kimbari

Sylvanus Karemera15 Aprili 2021

Vyombo vya usalama nchini Rwanda vimetangaza kuwakamata watu 66 ndani ya juma moja lililopita wakati nchi hiyo ilipokuwa kwenye kipindi cha maombolezo ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo miaka 27 iliyopita. Shirika la upelelezi la Rwanda limesema watu hao wanashukiwa kufanya vitendo vya kubeza kutokea kwa mauaji hayo pamoja na kuhatarisha maisha ya walionusurika.

https://p.dw.com/p/3s3qD

Vyombo vya usalama nchini Rwanda vimetangaza kuwakamata watu 66 ndani ya juma moja lililopita wakati nchi hiyo ilipokuwa kwenye kipindi cha maombolezo ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo miaka 27 iliyopita.

Shirika la upelelezi la Rwanda limesema watu hao wanashukiwa kufanya vitendo vya kubeza kutokea kwa mauaji hayo pamoja na kuhatarisha maisha ya walionusurika. Kutoka Kigali mwandishi wetu Sylivanus Karemera anaripoti zaidi

Kwa kawaida vitendo vya aina hii vimekuwa vikijitokeza hasa wakati wa juma la maombolezo kuwakumbuka waathirika wa mauaji hayo yaliyofanyika Rwanda mwaka 1994.

Shirika la upelelezi na makosa ya jinai la Rwanda limesema orodha ya watu 66 ndiyo waliokamatwa wakati siku saba za juma hilo la maombolezo na hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya Rwanda, baada ya kufanya vitendo kadhaa ambavyo kisheria vilionekana kuwa na uhusiano wa kupinga kutokea kwa mauaji hayo au vyenye mwelekeo wa kuendeleza chuki ya mauaji hayo.

Manusura wa mauaji wasimulia walichoshuhudia 

Ruanda 25. Jahrestag des Völkermords an der Gedenkstätte „Kigali Genocide Memorial“ in Gisozi, Kigali
Picha: Getty Images/AFP/B. Doppagne

Baadhi ya manusura wa mauaji hayo ya kimbari kama Bi Mukamurenzi Hilarie wameshuhudia kilichowatokea kabla ya watu hao kukamatwa.

"Ile asubuhi tulipoamka, mume wangu alikuwa pembeni akiwalisha ng'ombe na mtoto wetu alipoteremka shambani alikuta migomba yetu yote imefyekwa  na kurudi akikimbia na kumuuliza babake kama ndiye alikuwa ameikata migomba hiyo,lakini babake akakana na yeye alipokwenda kushuhudia kweli akaikuta migomba yote iko chini." amesema Hilarie.

Manusurika wengine wameshuhudia kwamba waliona mambo yasiyo ya kawaida siku ya kwanza ya  juma la maombolezo.

Huyu hakutaka jina lake kutajwa amesema "Kuna kisa kimoja ambacho tulimshuhudia mtu akiwaacha mto barabarani na kuzuia wapita njia, na alipoulizwa kile alichokuwa akikifanya, alijibu alikuwa akifanya ishara ya kuwambuka ndugu zake kutoka kabila lake la wahutu waliouawa kwenye mauaji hayo ya kimbari dhidi ya  watutsi wa Rwanda."

Manusura huuwawa kila maadhimisho yanapokaribia 

Frankreich, Paris: Anhörung von Felicien Kabuga zum Völkermord von Ruanda
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Mauaji yaliyofanyika Rwanda mwaka 1994 umoja wa mataifa ulithibitisha kwamba yalilenga kuitokomeza jamii ya watutsi huku yakifanywa na wanamgambo kutoka kabila la wahutu walio wengi.Lakini kila shughuli za maombolezo zinapoanza visa vya kuwaua manusura kutoka kabila la watutsi walio wachache hujitokeza.

Msemaji wa shirika la upelelezi na makosa ya jinai nchini Rwanda Dr Thierry Murangira amesema kutokana na visa hivyo tayari wanawashikilia washukiwa 66 wa makosa hayo.

Hata hivyo haya yanajiri wakati takwimu za tume ya taifa ya umoja na maridhiano zikionyesha kwamba kiwango cha maridhiano miongoni mwa wanyarwanda kipo kwenye uwiano wa asilimia 92%, huku lakini wadadisi wakijiuliza uhakika wa takwimu hizi ikiwa visa vya aina hii vikiendelea kuwepo tena kwa wingi.

Wenyewe wanasema watu hao wakikutikana na hatia wanakabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha jela.