1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda yakosolewa kwa vitisho na mauaji ya wakosiaji ugenini

Josephat Charo
10 Oktoba 2023

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema serikali ya Rwanda imewaua, kuwashambulia na kuwapoteza wakosoaji nje ya mipaka ya nchi.

https://p.dw.com/p/4XLHo
Rwanda, taifa dogo la Afrika Mashariki limekuwa likiongozwa na rais Paul Kagame tangu mauaji ya halaiki ya 1994, na anapania kuendeleza utawala wake.
Rwanda, taifa dogo la Afrika Mashariki limekuwa likiongozwa na rais Paul Kagame tangu mauaji ya halaiki ya 1994, na anapania kuendeleza utawala wake.Picha: Dan Kitwood/POOLAFP

Kulingana na shirika hilo, hayo ni sehemu ya kampeni ya ukandamizaji ambao sharti ukabiliwe na jumuiya ya kimataifa.

Taifa hilo dogo la Afrika Mashariki limeongozwa na rais Paul Kagame tangu mauaji ya halaiki ya 1994 na anapania kuendeleza utawala wake katika uchaguzi mwaka ujao.

Katika ripoti yake mpya iliyochapishwa leo shirika la Human Rights Watch limesema ili kuendeleza udhibiti wa madaraka chama tawala cha Rwandan Patriotic Front kimechukua hatua za kutumia nguvu na machafuko kwa kitisho chochote dhidi ya mamlaka yake.

Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani pia limesema hatua hizo hazikuwalenga tu wakosoaji na wapinzani ndani ya nchi.

Shirika hilo liliwahoji watu zaidi ya 150 katika ripoti yake inayoijumuisha miaka tangu Kagame alipochaguliwa katika uchaguzi wa 2017.