1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda : sekta ya kisheria hatiani katika kupokea rushwa

Janvier Popote15 Desemba 2021

Mahakimu na waendesha mashtaka nchini Rwanda ndio wamepokea kiasi kikubwa cha rushwa,inaelezea ripoti mpya ya Shirika la Transparency International Rwanda.

https://p.dw.com/p/44JTr
Ruanda | Emmanuel Macron in Kigali | Paul Kagame
Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Wanyarwanda wengi wanaamini kwamba serikali inajitahidi kupiga vita rushwa lakini kiwango cha uaminifu kimeshuka tkutoka asilimia 81 nukta 9 mwaka 2019 hadi asilimia 71 nukta 9 mwaka huu wa 2021, haya ni kwa mujibu wa utafiti uliowahusisha wananchi 2,420 kutoka wilaya 11.

Kiasi cha wastani cha rushwa ambacho kilitolewa mwaka huu nchini Rwanda ni faranga elfu hamsini huku maeneo yaliyozongwa na rushwa yakiwa ni sekta Binafsi, Jeshi la Polisi kitengo cha usalama wa barabarani, Shirika la Viwango, Wizara ya Elimu na Serikali za Mitaa.

Ushirikishwaji wa kila mtu katika vita hii

Bi Ingabire Marie Immaculee ni Mwenyekiti wa shirika hilo, anasema ingawa Rwanda inatambulika kimataifa kama nchi ambayo imepanda ngazi nyingi katika vita dhidi ya rushwa ambapo kwa sasa ndio inaongoza kwa nchi za Afrika Mashariki, lakini ina kila sababu ya kuendelea kupambana.

''Kutokana na utashi wa kisiasa uliopo na hata mfumo wa sheria unaowabana wala rushwa, serikali imejitahidi sana lakini safari bado ndefu. Hatutakiwi kufanya sherehe kufurahia mafanikio haya ama kujilinganisha na nchi ambazo zinavuta mkia, kunahitajika ushirikishwaji wa kila mtu katika vita hii.",aliesema Ingabire.

Soma pia: Rwanda yawakamata watu 4 kwa kujaribu kutorosha pembe za ndovu

Hatua kali dhidi ya wahusika 

Gacaca Gericht in Ruanda
Picha: AP

Mahakimu na waendesha mashtaka, pamoja na kwamba siyo wengi wao walipokea rushwa kama ilivyo kwa sekta zingine, lakini wachache waliohongwa walipewa kiasi kikubwa zaidi. Hakimu alihongwa 327,000Rwf huku mwendesha mashtaka akipata faranga laki mbili, kulingana na ripoti hii.

Bwana Harron Mutabazi ni msemaji wa Mahakama za Rwanda. Amesema anakiri mahakamani kuna rushwa lakini zimechukuliwa hatua kali dhidi ya mahakimu wasiotii maadili ya taaluma yao.

"Ripoti yetu ya kuanzia mwaka 2005 inaonesha wamefutwa kazi mahakimu na makarani wapatao 50 kutokana na rushwa, na baadhi walihukumiwa vifungo, ikiwa na maana kwamba vita dhidi ya rushwa mahakamani ni safari endelevu.", alisema Mutabazi.

Soma pia: Wasiwasi juu ya Rwanda kupanua ushawishi wake Afrika:

Ripoti hii inaonesha asilimia 89 ya watu walijua kuhukusu kutokea vitendo rushwa lakini hawakuripoti matukio hayo kwa kuhofia kufuatiliwa, asilimia 22 wamesema hawakuona sababu yoyote ya kuripoti, asilimia 21 wanaamini kwamba hata wangeripoti zisingechukuliwa hatua zozote huku asilimia 16 ya watu wakmesema hata yule ambaye wangeripoti kwake walijua kuwa na yeye ni mla rushwa.