1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda kuimarisha lugha ya Kifaransa

Sylivanus Karemera25 Oktoba 2018

Serikali ya Rwanda imetangaza tena kuimarisha lugha ya Kifaransa shuleni na hata kwenye sehemu za biashara na mawasiliano mengine nchini humo.

https://p.dw.com/p/37CoV
Deutschland Louise Mushikiwabo bei Conflict Zone in Berlin
Picha: DW

Serikali ya Rwanda imetangaza tena kuimarisha lugha ya Kifaransa, miaka michache baada ya lugha hiyo kuonekana kupuuzwa nchini humo.Rwanda imefanya hivyo baada ya waziri wake wa mashauri ya kigeni Bi Louise Mushikiwabo kuchaguliwa kuwa katibu mkuu wa shrikisho la mataifa 88 yanayozungumza lugha ya kifaransa ulimwenguni.

Uamuzi huu umetangazwa usiku wa kuamkia leo kwenye baraza la mawaziri lililoongozwa na Rais Paul Kagame mwenyewe. Taarifa ya baraza la mawaziri imesema kwamba baraza hilo limeidhinisha kwa kauli moja kuimarisa matumizi ya lugha ya kifaransa mashuleni, kwenye mafunzo ya aina zote na hata kwenye sehemu za biashara na mawasiliano mengine.

Hatua hii inakuja miaka kadhaa baada ya lugha ya Kifaransa kuonekana kama inapungua umuhimu wake licha ya katiba ya Rwanda kuikubali kama mojawapo ya lugha rasmi nchini Rwanda ikiwa ni pamoja na Kinyarwanda, Kiingereza,na Kiswahili.

Kifaransa kilisahaulika?

Waziri sheria akiwa pia mwanasheria wa serikali Johnston Busingye amesema.

"Wanyarwanda ni lazima waelewe tena umuhimu na maatumizi ya lugha ya Kifaransa, tulichokifanya hapo awali ni kwamba tuliamua kuimarisha lugha ya Kiingereza ambayo kihistoria ilikuwa kwenye kiwango cha sifuri katika nchi yetu lakini si kwamba tulipiga marufuku Kifaransa kama ambavyo mmekuwa mkisikia."

Kiswahili, Kingereza, Kifaransa na Kinyarwanda zitakuwa zinafundishwa kwa kiwango sawa nchini Rwanda
Kiswahili, Kingereza, Kifaransa na Kinyarwanda zitakuwa zinafundishwa kwa kiwango sawa nchini RwandaPicha: DW/A. Koch

Haya yanajiri siku chache baada ya aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Bi Louise Mushikiwabo kuchaguliwa katibu mkuu wa shirikisho la mataaifa yanayotumia lugha ya Kifaransa katika uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu huko nchini Armenia. Baadhi walichukulia uamuzi huu wa Rwanda kama jitihada za kufufua lugha hii. Hata hivyo waziri wa nchi katika wizara ya elimu Dkt. Isaac Munyakazi ametupilia mbali mtazamo huo.

Rwanda kuwa na lugha nne zinazofundishwa shuleni

"Haina maana lugha hii haikuwepo na wala haina uhusiano wa kuchaguliwa kwa Waziri Mushikiwabo hapana huo ni uzushi mtupu na ndiyo maana tunasema tunaimarisha. Kuimarisha maana yake ni unaimarisha kitu ambacho kilikuwepo. Jjitihada hizi ni mojawapo ya mchakato mzima wa kutathmini jinsi lugha zinavyofundishwa kuanzia kule chini."

Lakini wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lycee de Kigali jijini Kigali wametoa maoni tofautitofauti. Mmoja amesema "Masaa ya kujifunza kifaransa yalikuwa machache ikiliganishwa na yale ya kiingereza." mwenzake mwengine naye ameongeza akisema: 

"Ilikuwa haitoshi kwa muda tuliokuwa tunajifunza lakini kwa vyovyote tulijitahidi kuzingatia hayo tulokuwa tunafundishwa."

Kwa uamuzi huu sasa ni dhahiri kwamba lugha nne za Kiswahili, Kingereza, Kifaransa na Kinyarwanda zitakuwa zinafundishwa kwa kiwango sawa nchini Rwanda hali inayowapa wanafunzi fursa kwenye lugha hizi muhimu ulimwenguni.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga