1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto atoa amri ya mabadiliko ya utendakazi wa wizara Kenya

10 Januari 2023

Rais William Ruto wa Kenya ametoa amri ya mabadiliko ya utendakazi wa wizara za serikali ya nchi hiyo, kwa kuhamisha baadhi ya vitengo na kufafanua majukumu ya naibu Rais na Mkuu wa mawaziri.

https://p.dw.com/p/4LweV
Kenia Nairobi | Feier am Mashujaa Day
Picha: Simon Maina/AFP

Wizara zilizofanyiwa mabadiliko katika amri ya kwanza ya Rais ya mwaka 2023, ni pamoja na wizara za maji, ardhi, afya na uchukuzi. Kulingana na amri mpya ya Rais, Mamlaka ya uchukuzi nchini NTSA, imehamishwa kutoka wizara ya usalama na kupelekwa kwenye wizara ya uchukuzi na itakuwa chini ya Waziri Kipchumba Murkomen.

Akizingatia ahadi yake ya kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa na mabadiliko ya tabia nchi, Rais Ruto amebuni kitengo maalum kwenye wizara ya mazingira ambacho ni idara ya mazingira na tabia nchi. Katika wizara ya afya, Rais amefafanua majukumu kati ya katibu wa idara ya huduma za afya na idara ya afya ya umma na ubora wa taaluma ili kulainisha shughuli za serikali. Mwanasheria mkuu Justin Mturi, ana jukumu la kuhakikisha masuala yanayohusu idara ya mahakama yanashughulikiwa.

DW-Interview Wycliffe Musalia Mudavadi, kenianischer Politiker
Mkuu wa Mawaziri Kenya Musalia MudavadiPicha: DW/S. Wasilwa

Pamoja na hayo, mabadiliko haya yamefafanua majukumu kati ya naibu Rais Rigathi Gachagua na Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi. Afisi ya waziri kiongozi imejumuishwa kwenye afisi ya Rais ambako itahudumu na afisi ya naibu wa Rais. Majukumu yatakayoendeshwa na naibu Rais ni pamoja na kusimamia shughuli na kufanya mabadiliko katika sekta ya kahawa, kuongoza kamati za mabaraza ya mawaziri, kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo yake, kuratibu mipango ya maendeleo na washirika wa kigeni na kusimamia tume ya mito ya Nairobi. Mwenzake Musalia Mudavadi atasimamia shughuli za makatibu wa wizara zote na ataongoza shughuli ya kuratibu ajenda za serikali kwenye bunge kuhakikisha miswada muhimu inapewa uzito.

Hatua hii ya Rais kuorodhesha bayana majukumu ya viongozi hawa wawili inaonekana kama nia ya kukomesha uhasama uliokuwa unatokota kati yao. Musalia Mudavadi ameonekana kupinga cheche anazozitoa naibu Rais Rigathi kwenye mikutano ya umma, akisisitiza haja ya kuhimiza utangamano na kuganga yajayo.

Rigathi vile vile amekosolewa kwa kutofautiana na utendaji kazi wa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Hata hivyo, wachambuzi wanahoji kwamba baadhi ya majukumu yaliyopewa afisi ya Rais, yanakinzana na majukumu yanayotekelezwa na wizara mbalimbali. Anaporatibu mageuzi na mipangilio ya kulainisha shughuli za serikali, Rais William Ruto amewataka maafisa wake kutoka huduma kwa umma ipasavyo, akionya dhidi ya utepetevu.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru