1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RUMBEK : Garang kuzikwa leo wakati Uganda ikihoji kifo chake

6 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CEnf

Kiongozi wa zamani wa waasi nchini Sudan John Garang leo anatazamiwa kuzikwa lakini hali ya mashaka juu ya kile kilichosababisha kifo chake kufuatia mkataba wa kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu kabisa barani Afrika imeweka kiwingu juu ya maziko hayo.

Kifo cha Garang katika ajali ya kuanguka kwa helikopta ikiwa ni wiki tatu tu baada ya kuapishwa kuwa Makamo wa Rais wa Sudan kimezusha ghasia mjini Khartoum na kusababisha watu 130 kuuwawa na kuzusha hofu kwamba makubaliano hayo ya kukomesha vita hivyo vya miaka 21 yumkini yakasambaratika.

Kifo chake cha ghafla kilimfadhaisha mpiganaji wa zamani wa chini kwa chini na rafiki yake wa karibu Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye hapo jana amesema yumkini kifo chake hicho hakikusababishwa na ajali na kwamba kulikuwa na mkono wa nje.

Kumekuwepo na tetesi kubwa kusini mwa Sudan kwamba helikopta ya Rais huyo wa Uganda iliokuwa imechukuwa Garang ilikuwa imehujumiwa au imetunguliwa.Uchunguzi huru wa kimataifa utaanzishwa kuyakinisha kuanguka kwa helikopta hiyo.

Takriban watu nusu milioni wanatarajiwa kuhudhuria mazishi yake katika mji mkuu wa muda mrefu wa Sudan ya kusini wa Juba ngome muhimu ya kivita ya serikali ambao waasi wa chama chake cha SPLA walipigana vikali kuuteka bila ya mafanikio wakati wa vita vyao.