1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ronaldo aandika historia tena

22 Aprili 2019

Cristiano Ronaldo ameandika historia kwa mara nyengine tena kwa kuwa mchezaji wa kwanza kushinda ligi tatu kuu za Ulaya. Nyota huyo wa Juventus amepata hadhi hiyo baada ya klabu yake kunyakua ubingwa wa Serie A.

https://p.dw.com/p/3HDuN
Fußball |  Juventus Turin vs AC Florenz | Ronaldo
Picha: imago//ImagePhoto/M. Gribaudi

Juventus iliifunga Fiorentina 2-1 siku ya Jumamosi.

Sasa Ronaldo mwenye umri wa miaka 34 na ambaye amenyakua tuzo ya mchezaji bora duniani mara tano ameshinda ligi kuu ya England, La Liga ya Uhispania na hiyo ligi ya Italia.  Kuna wachezaji wengine ambao wamewahi kuwa mabingwa katika ligi tano kuu za Ulaya ila hakuna ambaye ashawahi kushinda ligi hizo tatu kuu, ya England, Uhispania na Italia.

David Beckham aliwahi kushinda ligi ya England, Uhispania na Ufaransa ingawa hakushinda Serie A ya Italia alipokuwa kwa mkopo AC Milan.

Kocha wa Juve Massmiliano Allegri ameonyesha furaha kwa klabu yake kunyakua ubingwa kwa mara ya nane mfululizo hasa baada ya kubanduliwa kwenye ligi ya vilabu bingwa Ulaya na Ajax Amsterdam wiki iliyopita.

"Leo ni siku njema sana, nayaweka kando kabisa yale ya kuondolewa kwenye Champions League kwasababu tulivunjika moyo sana na kuwa wenye uchungu. Bahati nzuri tulikuwa na hii mechi ya leo siku tatu baadae," alisema Allegri.