1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya MH17 haina majibu ya kutosha

Elizabeth Shoo10 Septemba 2014

Mada kuu zinazojadiliwa na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi Ujerumani pamoja na ripoti kuhusu ajali ya ndege ya Malaysia Airlines MH17.

https://p.dw.com/p/1D9lU
Mabaki ya MH17
Picha: picture-alliance/dpa

Chama cha CSU kinachotawala kwenye jimbo la Bavaria kimetishia kuanzisha ukaguzi kwenye mpaka wa jimbo hilo na nchi jirani ili kuzuia wakimbizi wasiingie. Kuhusu mpango huo wa chama cha CSU, gazeti la "Main-Post" linaandika: "Mwaka 1992 jimbo la Bavaria liliwapokea wakimbizi 90,000 na mwaka huu inakadiriwa kwamba idadi ya wanaotafuta hifadhi jimboni hapo ni watu 33,000. Bavaria haitashindwa kuwahudumia watu hao, tena ikizingatiwa kwamba ni moja ya majimbo tajiri zaidi Ujerumani."

Mhariri wa gazeti la "Nürnberger Zeitung" anawasifu raia wa Ujerumani kwa kuchukua hatua wakati ambapo wanasiasa bado wanalumbana. Mhariri wa gazeti hilo anasema: "Wakati huu tunashuhudia kwamba wananchi wengi wanawaunga mkono na kuwasaidia wakimbizi. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria na tishio la Dola la Kiislamu huko Iraq ni mambo yanayotufanya tuthamini amani na utajiri tulionao hapa nchini."

Ndugu wa wahanga waambiwe ukweli

Mada nyingine iliyopewa uzito ni ripoti iliyotolewa jana juu ya kuanguka kwa ndege ya Malaysia Airlines MH17. Gazeti la "Straubinger Tagblatt" linaandika: "Ndugu na marafiki wa watu waliopoteza maisha yao kwenye ajali hiyo hawataridhishwa na ripoti iliyotolewa The Hague hapo jana." Mhariri wa gazeti hilo anaendelea kusema kwamba wanachohitaji ndugu na marafiki hao ni uhakika juu ya kisa cha ajali hiyo. Lakini inaelekea kuwa itabidi wakubaliane na ukweli kwamba vifo vya abiria waliopanda ndege hiyo vilikuwa matokeo ya kosa lililotokea katika eneo la vita.

Wahanga wa MH17 wakipewa heshima za mwisho
Wahanga wa MH17 wakipewa heshima za mwishoPicha: Reuters

Naye mhariri wa gazeti la "Lübecker Nachrichten" anawanyooshea kidole wahusika wote wa ajali hiyo kwa kutupiana lawama. Mhariri huyo anaandika: "Nchi za Magharibi zinaichukulia ripoti juu ya ajali kama ushahidi kwamba Malaysia Airlines MH17 ilidunguliwa na kombora lililotengenezwa Urusi. Waasi wa Ukraine wanaotaka kujitenga, kwa upande wao wanailaumu serikali ya Kiev. Na Urusi kama kawaida inadai kuwa haina kosa lolote huku ikikosoa kuwa ripoti juu ya ajali haikuwa na taarifa za kutosha. Lakini ndugu wa wahanga wa ajili hiyo wana haki ya kufahamu ni nani hasa mwenye makosa."

Wengi wakimbilia vyuoni

Mada ya mwisho ni ripoti ya jumuiya ya ushirikiano na maendeleo ya kiuchumi, OECD, kuhusu viwango vya elimu katika nchi za Ulaya. Ripoti hiyo inaonyesha kwamba hapa Ujerumani, mshahara wa mtu mwenye shahada ya chuo kikuu ni asilimia 74 zaidi ya ule wa mtu asiye na shahada.

Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linakumbusha kwamba hiyo ni sababu inayoifanya serikali iwahimize wengi kusoma chuo kikuu. Lakini serikali haijaweka mazingira mazuri kwa wanafunzi: Vyuo vikuu vimejaa na watu wanaotaka kusoma wanakosa nafasi. Wakati huo huo kuna uhaba mkubwa wa wanafunzi kwenye shule za ufundi.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga