1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti: Ulawiti wa wavulana waibua wasiwasi Rwanda

Sylvanus Karemera26 Februari 2021

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya makosa ya jinai nchini Rwanda imeonesha hali ya wasiwasi kutokana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia hasa watoto na vijana wa kiume kufayiwa vitendo vya ulawiti.

https://p.dw.com/p/3pyVy
Afrika | Motorradfahrer mit einem Trikot der deutschen Fußball-Nationalmannschaft in Ruanda
Picha: picture-alliance/dpa/imageBROKER

Baadhi ya waathirika wametoa ushuhuda wa kusikitisha baada ya kuambukizwa magonjwa sugu kama vile virusi vya ukimwi (VVU) na maradhi mengine kutokana na vitendo hivyo. 

Kijana mmoja wa miaka 18 ambaye tumempa jina la bandia la Jean Claude, anasema alianza kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji mathalan kulawitiwa alipokuwa na umri wa miaka 14.


"Nilikuwa nimetoka nyumbani masaa ya jioni nikienda bomba kuchota maji na nilipokuwa njia kurejea nyumbani nilikutana na mtu mmoja akaniomba kunisaidia kubeba. Niliona anachomoa kisu akaniamuru kulala chini na akasema nikipiga kelele atanichoma, alivua nguo kisha akanivua na kunipaka mafuta katika sehemu ya kutolea haja kubwa na akafanya mambo yake. Siku hiyo niliumia na nilipofika nyumbani sikusema chochote."

Kijana mwingine ambaye tumempa jina la bandi la Frank mwenye umri wa miaka 19, yeye alianza kulawitiwa akiwa na umri wa miaka 13:

"Huyu alikuwa jirani na nyumbani, mara ya kwanza alinipeleka kwake akataka kunilawiti nikakimbia, lakini mara ya pili aliniambia kulikuwa na hafla pale kwao na kweli nikaenda na kuwakuta vijana wengine. Tulikunywa na ilipofika usiku tukaamua kulala pale, usiku akaingia chumba nilichokuwa nimelala na kunilawiti. Nilijaribu kupiga lakini kwa sababu alinizidi nguvu sikufanikiwa kuomba msaada, hadi mwisho nilizirai kwa maumivu."
 

Mmoja wa vijana hao amesema mwisho alipata uraibu wa kulala na wanaume wenzie hadi kuambukia virusi vya Ukimwi. Kwa kauli moja wanasema ilifikia hatua wote kila mmoja akafukuzwa kutoka familia yao kutokana na jinsi walivyoanza kunyanyapaliwa. Idadi kubwa ya vijana wanaofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia huficha matatizo waliyoyapata suala ambalo linatajwa kama linalochangia uzito wa tatizo hilo nchini Rwanda.

Taasisi ya taifa ya makosa ya jinai RIB imetoa ripoti inayoonyesha visa 111 vya vijana wa kiume walionyanyaswa kijinsia mwaka 2019/20.
Taasisi ya taifa ya makosa ya jinai RIB imetoa ripoti inayoonyesha visa 111 vya vijana wa kiume walionyanyaswa kijinsia mwaka 2019/20.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Hata hivyo wanasaikolojia wanasema licha ya kwamba watu wa aina hii wanakuwa na matatizo ya kuharibika kimaono lakini bado kuna nafasi japo kidogo ya kuerejea katika maisha ya kawaida. Bi Gerturde Nyirahabineza hufanya kazi ya kutoa ushauri nasaha kwa watu walio na matatizo ya aina hiyo.

"Mtu anapofanyiwa vitendo kama hivi vya matumizi ya nguvu maisha yake huharibika na ndiyo maana utawaona wengi wao wakionekana wenye upweke wa kupindukia, anajisahau na kujiona kama vile hafai tena katika jamii. Inapofikia hali hiyo sisi tunachokifanya tunawasogelea na kuzungumza nao, tunawasikiliza. Kimsingi tunawaambia kwamba jamii bado inawapenda na kuwathamini. Wengi wao pia wanakuwa na chuki kwa wazazi wao au ndugu zao kwa sababu ya kuwafukuza."

Kwa upande mwingine James Ndahayo kutoka kituo cha taifa cha malezi na makuzi kwa watoto amesema wazazi ndio wenye jukumu la awali kabisa la kuhakikisha usalama wa watoto wao.

"Ni vizuri wazazi kufuatilia makuzi ya watoto wao kila siku tena kwa makini,najua wazazi wengi huamkia huku na kule wakitafuta riziki lakini hata wakirejea nyumbani usiku ni lazima wapate muda wa kuzungumza na watoto wao. Hawapaswi kumuamini kila mtu hapana, hata mfanyakazi wa nyumbanai ni lazima ufuatilie ujue anashinda namna gani na watoto wako. Ni lazima ujenge urafiki na mwanao ili upate kuzungumza naye kuhusu kilichomsibu kutwa nzima." Amesema James.

Mpaka sasa serikali imeweka sheria kali zinazoadhibu watu wanaojihusisha na vitendo hivyo hadi kifungo cha maisha jela, lakini mpaka sasa vitendo hivyo vinaendelea kupanda.
 

Taasisi ya taifa ya makosa ya jinai RIB imetoa ripoti inayoonyesha visa 111 vya vijana wa kiume walionyanyaswa kijinsia mwaka 2019/20.

Mwezi uliopita mahakama mjini Kigali ilikumhuku kwenda jela maisha mwanaume mmoja baada ya kukutikana na hatia ya kuwanyanyasa watoto wa kiume 17 kwa nyakati tofauti.