1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa juu hali ya kiuchumi mwaka 2005 yatolewa

25 Januari 2006

Kinyume na matarajio,ongezeko kubwa la bei ya mafuta halijaleta athari zozote za kuuharibu uchumi unaoyumbayumba wa mataifa yanayoendelea

https://p.dw.com/p/CBJH

Kulingana na uchunguzi katika ripoti hiyo yenye kurasa 160 juu ya hali ya kiuchumi na maendeleo mwaka 2005,bei ya mafuta inatarajiwa kubakia kuwa juu katika kipindi kijacho na athari zake katika maendeleo na mabadiliko itatofautiana kutoka nchi hadi nchi.

Bei ya mafuta ambayo ilikuwa ni kiasi cha dalla 20 kwa pipa katika kipindi cha miaka ya tisini kuanzia wiki iliyopita ilipanda na kufikia hadi dalla 64 lakini hata hivyo inatarajiwa bei hiyo kushuka na kufikia dalla 60 kwa kila pipa mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo bei ya mafuta kimataifa ambayo imefikia asilimia 42 iko juu kuliko mwaka 2004 kwa wastani.Mapato yaliyopatikana kwa jumla katika nchi zote zenye utajiri wa bidhaa ya mafuta katika mashariki ya Kati inakadiriwa kufikia kiasi cha Dolla billioni mia tatu katika mwaka 2005.

Kiwango kinachtarajiwa katika mwaka 2006 huenda kikabaki kwa wastani katika kiwango cha mwaka uliopita licha ya kwamba wizara ya nishati nchini Marekani imetabiri kuwa mapato yanaweza yakafikia Dolla billioni mia tano na ishirini na mbili mwaka huu na kuimarisha zaidi mapato ya nchi zinazotegemea mafuta katika uchumi wake.

Akiulizwa kwa nini mataiafa yanayoendelea hayalalamikii bei ya juu ya mafuta kama vile yalivyovafannya katika miaka ya sabini Rob Vos mkurugenzi wa sera za maendeleo na utafiti katika idara ya uchumi na masuala ya jamii kwenye Umoja wa Mataifa DESA alisema mengi ya mataifa hayo kwa sasa yananufaika kutokana na bei ya juu ya mafuta.

Akizungumza na shirika la habari la IPS bwana Vos aliongeza kusema kuwa mataifa hayo yananufaika ama kwa kutokana na wafanyibiashara wakubwa wa mafuta ama kutokana na bei za bidhaa zisizotokana na mafuta kuwa juu pamoja na bei za nyingi ya bidhaa zinazoingizwa katika nchi hizo kuwa chini. Kutoka na hilo nyingi ya nchi hizo zimefaidika.

Ukuaji mkubwa wa uchumi katika nyingi ya nchi zinazoendelea kwa kiasi kikubwa umeelezwa kwamba unatokana na bei nzuri ya bidhaa zinazouzwa nchi za nje.

Ripoti hiyo mpya ya Umoja wa mataifa pia inaeleza kuwa makampuni mengi yanayoagiza mafuta yanakumbwa na matatizo kidogo kutokana na bei ya mafuta kubakia juu na ruzuku mbali mbali amabazo serikali nyingi za mataifa yanayoendelea huweka katika bei ya nishati ambayo ni vigumu kuigharamia kwa hiyo,ongezeko la bei ya mafutalinahamishiwa kwa watumiaji na kusababisha gharama katika uzalishaji

Ripoti hiyo ya kila mwaka inaonyesha kuwa hata hivyo matatizo kadhaa yanakabili ukuaji wa uchumi katika mwaka 2006. Bei ya juu ya mafuta amabyo itaendelea kwa muda mrefu na kuchukua zaidi ya mwaka mmoja huenda ikaleta athari kubwa ya ughali wa maisha katika uchumi wa mataifa mengi ya Afrika.

Licha ya kwamba ripoti hiyo inasema kuwa bei ya juu ya mafuta inaleta athari kubwa katika mataifa yanayoagiza mafuta mengi ya mataifa hayo yamechukua hatua za kuwalinda wateja kwa kuanzisha ama kuimarisha udhibiti wa bei ya nishati na ruzuku.

Kwa kiwango kikubwa ripoti hiyo imesema ukuaji wa uchumi wa dunia ulianza kupungua kasi kwa kiwango kikubwa katika mwaka 2005 kutoka kasi kubwa ya ukuaji mwaka 2004. Uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kukuwa katika kasi hii ya wastani ya kiwango cha asilimia 3 katika mwaka wa 2006.

Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na wastani wa miaka kumi iliyopita.

Hata hivyo kwa wastani inasema ripoti hiyo uchumi wa mataifa yanayoendelea unatarajiwa kukua kwa kiwango cha asilimia 5.6 na katika uchumi wa mataifa yaliyofanya mageuzi kwenye uchumi wao ukuaji utakuwa kwenye kiwango cha asilimia 5.9,licha ya ukweli kwamba uchumi wa mataifa haya unaweza ukakumbwa na changamoto kubwa katika mwaka 2006.

Wakati China na India kwa kiasi kikubwa ndio nchi zenye uchumi unaokuwa kwa haraka mataiafa yaliyobaki ya kusini na mashariki ya Asia yanatarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia tano.

Mataifa ya Amerika ya kusini kwa upande mwingine yanabaki kuwa nyuma yakiwa na ukuaji wa asilimia tatu na nukta tisa.

Lakini ukuaji wa uchumi wa mataifa ya Afrika unatarajiwa kubaki katika kiwango cha asilimia tano.

Hata kama viwango hivyo vya juu vitaendelea ripoti hiyo inasema ukuaji wa pato jumla la mataifa hayo bado halitokuwa imara vya kutosha katika nyingi ya nchi hizi ili kufanya kuimarisha maendelea kuelekea juhudi za kupambana na umasikini uliokithiri kufikia mwaka 2015.