1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya yazinduliwa

ELZABETH KEMUNTO7 Septemba 2004

Uwezekano wa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, umeonekana kuwa karibu zaidi, baada ya ripoti kuchapishwa kuhusu faida zitakazotokana na kujiunga kwake.

https://p.dw.com/p/CEHc
Aliyekuwa rais wa Finland Martti Ahtisaari ndiye mwenye kiti wa kamati iliyotoa ripoti ya kuunga mkono Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya
Aliyekuwa rais wa Finland Martti Ahtisaari ndiye mwenye kiti wa kamati iliyotoa ripoti ya kuunga mkono Uturuki kujiunga na Umoja wa UlayaPicha: AP

Ripoti hiyo imechapishwa huku kamishna wa upanuzi wa Umoja wa Ulaya Guenther Verheugen, akisema kuwa hali ya haki za binadamu nchini Uturuki ni bora zaidi.

Wasiwasi kuhusu haki za binadamu, imekuwa kizuizi kikubwa kwa nchi hiyo wakati ikijaribu kujiunga na Umoja wa Ulaya. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na baraza tawala la Umoja huo, litatangaza mnamo tarehe 6 oktoba, kama linaamini kuwa Uturuki imetimiza masharti yanayotakikana, ili kuanza mazungumzo ya kuipatia fursa nchi hiyo. Viongozi wa Ulaya watazingatia ombi la Uturuki katika mkutano mkuu utakaofanyika kati ya tarehe 17 na 18 Desemba, ili kuamua ikiwa wataweka tarehe utakapoanza utaratibu huo.

Ripoti hiyo yenye kichwa "Uturuki katika Ulaya: Ni zaidi ya ahadi?", ilitoa pendekezo kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya kuanza mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja huo. Ripoti hiyo imezidi kueleza kwamba mazungumzo hayo yanaweza kuanza punde baada ya Uturuki kutimiza masharti ya Copenhagen, ambayo kila nchi lazima itimize kabla ya kujiunga kwao na Umoja huo kuzingatiwa.

Masharti haya ni pamoja na kuwa na sheria au desturi thabiti, demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu, kuwa na heshima na kuyalinda makundi yanayobaguliwa na kuwa na uchumi bora.

Ripoti hiyo imechapishwa na kamati huru ya Uturuki, ambayo wahusika wake ni marais wastaafu, mawaziri wa mambo ya nje na makimishna wa Umoja Ulaya. Kamati hiyo ilibuniwa mnamo machi mwaka huu ili kuelimisha mjadala kuhusu uwanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya.

Uturuki ina kila sababu ya kutarajia kupokewa na Umoja huo, bora tu itimize masharti yanayotakikana. Kamati iliyoandika ripoti hiyo inautaka Umoja wa Ulaya kuiheshimu Uturuki na kufikiria juu ya masuala yanayoihusu kwa haki.

Aliyekuwa rais wa Finland na ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, MAARTI AHTISAARI, alitaka uamuzi kufanywa haraka iwezekanavyo. Alisema hayo wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti hiyo mjini Brussels. AHTISAARI aliongeza kwamba kuchelewesha uamuzi kuhusu uturuki utaharibu sifa ya Umoja wa Ulaya. Uturuki imekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka ya hivi karibuni huku ikijaribu kutimiza masharti ya kisiasa yanayotakikana ili kuwa mwanachama wa Umoja huo.

AHTISAARI alisisitiza kwamba hofu ya Waturuki kuhamia Ulaya inafaa kufutiliwa mbali. Ripoti hiyo inatarajia kuwa kama Uturuki itapewa uwanachama wa Umoja wa Ulaya, wahamiaji milioni 2.7 watasafiri kutoka Uturuki hadi nchi zingine za Umoja huo, lakini hiyo itakuwa ni asilimia 0.5 ya idadi yote ya nchi za Umoja wa Ulaya. Waturuki wapatao milioni 3.8 tayari wanaishi Ulaya.

Ripoti hiyo ilikiri kuwa kutakuwa na matatizo ya kuijumuisha nchi kubwa kama vile Uturuki katika utaratibu wa kufanya uamuzi katika Umoja wa Ulaya, lakini hakuna kitu hakiwezekani.

Uturuki ina idadi ya watu milioni sabini, na idadi hii inaweza kulinganishwa na idadi ya watu katika nchi zote kumi za Umoja wa Ulaya. Vile vile kuna wasiwasi kwamba kuingia kwa waislamu milioni sitini na sita katika umoja huo, kutabadilisha sura ya Umoja wa Ulaya.

Ripoti hiyo mpya pia inasema kwamba utamaduni wa uturuki huenda ukawa wa manufaa kwa Umoja huo katika mashariki ya kati, mbali na kuboresha uhusiano na mataifa ya kiislamu.

Licha ya ukubwa wake na sifa zake za kipekee na uhakika ya kwamba Uturuki itakuwa aina tofauti ya mwanachama, nchi hiyo haina uwezekano wa kuibadilisha misingi ya Umoja huo.

Kamati iliyotoa ripoti hiyo imekubaliana kwamba kuna msingi wa kutosha wa kufanya uamuzi wa mwisho.