1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelenskiy ataka mazungumzo ya kina na Moscow

Sylvia Mwehozi
19 Machi 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametoa wito hii leo wa mazungumzo ya kina ya amani na Moscow, akisema ndiyo nafasi pekee ya Urusi kupunguza uharibifu uliotokana na makosa yake baada ya kufanya uvamizi.

https://p.dw.com/p/48iRm
Bildkombo | Wladimir Putin und Wolodymyr Selenskyj
Picha: A. Gorshkov/SPUTNIK/AFP/Getty Images/Presidency of Ukraine/AA/picture alliance

Zelenskiy amesema Ukraine imekuwa ikitoa suluhisho kila wakati la amani na kutaka mazungumzo yenye maana  juu ya usalama bila kuchelewa.

Kulingana na Zelenskiy vikosi vya Urusi vinazuia kwa makusudi usambazaji wa misaada ya kiutu katika miji iliyoko chini ya mashambulizi.

Putin na Scholz wazungumza tena kuhusu Ukraine

Rais huyo amesema hadi sasa hakuna taarifa za watu wangapi wamefariki baada ya jumba la maonyesho kushambuliwa mjini Mariupol. Wakati huo huo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi katika miji ya Ukraine ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kyiv na kituo cha ukarabati wa ndege nje kidogo ya mji wa Lviv, karibu na mpaka na Poland.Urusi yaendeleza Mashambulizi Ukraine

Mjumbe wa Urusi katika mazungumzo na Ukraine ya kusaka suluhu ya vita inayoendelea Vladimir Medinsky amesema pande hizo mbili ziko karibu kuafikiana katika mambo muhimu juu ya uwezekano wa Ukraine kutoegemea upande wowote na uanachama katika jumuiya ya kujihami NATO, lakini bado kuna baadhi ya masuala hayajatatuliwa kabla ya marais wa nchi hizo mbili kukutana.

Rais Putin jana alijitokeza hadharani katika sherehe za kumbukumbu ya miaka nane tangu Urusi ilipoitwaa rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014. Putin alitumia sherehe hizo kusifu vikosi vyake vinavyopigana huko Ukraine. "Bega kwa bega, wanasaidiana,'' alisema Putin akiongeza kwamba nchi haijawahi kuwa na umoja kama huo kwa muda mrefu.

Putin pia amefanya mazungumzo kwa njia ya simu ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Ufaransa na kusisitiza kwamba Moscow inafanya kila linalowezekana kuepusha madhara kwa raia. Rais Macron wa Ufaransa ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya mji wa Mariupol ulioko mashariki mwa Ukraine ambao umezingirwa na vikosi vya Urusi, na kutoa wito wa kusitisha mapigano.

Gespräch von Biden und Xi
Rais wa Marekani Joe Biden na rais wa China Xi JinpingPicha: Liu Bin/Xinhua/dpa/picture alliance

Wakati huohuo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi katika miji ya Ukraineikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kyiv, na kukishambulia kituo cha ukarabati wa ndege nje kidogo ya mji wa Lviv, karibu na mpaka wa Poland.

Na Rais wa Marekani Joe Biden amemuonya mwenzake wa China Xi Jinping juu ya athari zitakazoikabili beijing endapo itaipatia msaada wa vifaa Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Jen Psaki amesema rais Biden ameelezea jitihada za Marekani na washirika wake katika kushughulikia uvamizi wa Urusi, ikiwemo kuiwekea vikwazo vikali Moscow. Aidha Biden amesisitiza utatuzi wa kidiplomasia katika mgogoro huo.

Nayo Wizara ya mambo ya nje ya China imesema kuwa rais Xi amemwambia Biden kwamba vita nchini Ukraine ni lazima ikomeshwa haraka iwezekanavyo na kutoa wito kwa jumuiya ya kujihami NATO kufanya mazungumzo na Moscow. Hata hivyo kiongozi huyo hajashutumu uvamizi huo wa Urusi kwa mujibu wa taarifa ya Beijing.