1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais Xi Jinping akubali kuzungumza na Zelensky

6 Aprili 2023

Ufaransa na Umoja wa Ulaya wamtia kishindo Xi Jinping airudishe Urusi kwenye mazungumzo kumaliza vita ya Ukraine lakini pia kutoipelekea silaha nchi hiyo

https://p.dw.com/p/4PnIs
Frankreichs Präsident Macron besucht China - von der Leyen
Picha: Ludovic Marin/Pool AFP/AP/dpa/picture alliance

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na rais wa Umoja wa Ulaya,Ursula von der Leyen wamefanya mazungumzo kwa pamoja na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing. Na  katika mazungumzo hayo Macron alimtolea mwito kiongozi huyo wa China kuishawishi Urusi kuachana na vita na kuwarudisha wadau wote kwenye meza ya mazungumzo.

Rais Emmanuel Macron amesema ana matumaini  China itaishinikiza Urusi kuingia kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Ukraine. Macron amesema uchokozi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha matatizo makubwa ya kiuthabiti duniani.Na kwahivyo amani ya kudumu inapaswa kufikiwa hivi sasa.

"Huu ndio msingi, kama tunavyoona katika kile ambacho tunapaswa kukitetea na ambacho kinahitaji hatua ya kurudi tena kwa mazungumzo  haraka iwezekanavyo ili  ipatikane amani ya kudumu.Lakini amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila ya watu wa Ukraine kuheshimiwa ambao ndio wenye kushambuliwa na bila ya Urusi kuonesha ushirikiano.

Macron ameongeza kusema kwamba wanachotaka sio tu mgogoro kumalizika bali iwepo heshima ya uhuru wa mamlaka na ardhi ya Ukraine likiwa ni sharti la kupatikana kwa amani ya kudumu. Kadhalika rais Macron amemshinikiza rais Xi Jinping kutoipelekea Urusi  chochote ambacho kinaweza kutumiwa katika vita dhidi ya Ukraine.

China Frankreich Emmanuel Macron Xi Jinping
Picha: Ng Han Guan/AP/picture alliance

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,Ursula von der Leyen kwa upande mwingine nae ameionya China kwamba kuipelekea silaha Urusi ni hatua itakayoharibu kwa kiwango kikubwa mahusiano na Umoja huo. Von Der Leyen amesema hayo kwenye mkutano na waandishi habari baada ya mkutano na rais Xi na waziri mkuu Le Qiang.

Wiki iliyopita von der Leyen alitowa tahadhari kwa Umoja wa Ulaya kujiweka tayari kuandaa hatua za kulinda biashara na uwekezaji ambao China inaweza kuutumia vibaya kwa maslahi yake ya kiusalama na kijeshi.

Kimsingi nchi za Magharibi zinakhofia kwamba Beijing inajiandaa kuipelekea Urusi silaha kuiunga mkono kwenye uvamizi wake nchini Ukraine.

Frankreichs Präsident Macron besucht China - von der Leyen
Picha: Ludovic Marin/Pool Photo via AP/picture alliance

Hata hivyo kwa upande wake rais Xi Jinping katika mkutano wake na Macron alisema atakuwa tayari kumpigia simu rais wa Volodymy Zelensky muda utakapofika, lakini pia yuko tayari kufanya kazi na Ufaransa kutia kishindo cha kufanyika mazungumzo ya kumaliza vita hiyo ya Ukraine kwasababu sera ya nchi yake kuhusu Ukraine ni kuunga mkono amani na mazungumzo.

"Katika suala la Ukraine,China inaendelea kutowa mwito wa mazungumzo ya kufikia maelewano. China iko tayari kufanya kazi na Ufaransa kuitolea mwito jumuiya ya kimataifa ijizuie kwa namna inayokubalika na kuepusha kuzidisha mgogoro,kuzuia hali kutofikia viwango vya kutodhibitika.Kuzingatia sheria ya kimataifa na kuepusha mashambulio yoyote dhidi ya raia.''

Xi Jiping pia ametahadharisha juu ya silaha za Nyuklia kutumika kwenye mgogoro huo akisisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kuzingatia  jukumu lake kuhakikisha silaha hizo hazitumiki kwa namna yoyote, na kupinga mashambulizi dhidi ya vituo vya nguvu za Nyuklia.

Miongoni mwa mengine pia yaliyojitokeza kwenye mkutano wa Beijing ni msimamo wa Ulaya kuhusu Taiwan,huku Ursula von der Leyen akiweka wazi kwamba  uthabiti wa kisiwa hicho ni muhimu na hakuna anayepaswa kuchukuwa uamuzi wa pekeyake kubadilisha hali iliyopo sasa kwa kutishia kutumia nguvu za kijeshi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW