1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Meli ya kwanza ya mizigo yaondoka Ukraine

17 Agosti 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesifu hatua ya kuondoka kwa meli ya kwanza ya mizigo kutoka nchini Ukraine kwa kutumia njia mpya ya Bahari Nyeusi baada ya Urusi kujitoa kwenye makubaliano ya nafaka.

https://p.dw.com/p/4VFzv
Meli ya mizigo na ya kwanza ya kiraia kuondoka nchini Ukraine kupitia Bahari Nyeusi baada ya Urusi kujitoa katika makubaliano ya nafaka
Urusi ilijiondoa kwenye makubaliano ya nafaka na kusema itazilenga meli zitakazopita kwenye Bahari Nyeusi Picha: Ukraine's Infrastructure Ministry Press Office/AP/picture alliance

Rais Volodymyr Zelensky amesema hayo wakati jumuiya ya kimataifa ikilaani vikali mashambulizi hayo ya karibuni ya Urusi kwenye bandari hizo, ikiionya Urusi kuacha kutumia chakula kama ngao ya vita. 

Rais Volodymyr Zelensky amesema Ukraine imefanikiwa kuchukua hatua muhimu kuelekea kurejesha uhuru wa kusafiri kupitia Bahari Nyeusi. Meli hiyo ya kiraia na ya kwanza kuondoka, imepitia njia mpya ya kiutu ya Ukraine, ikitokea bandari ya Odesa, licha ya maonyo kutoka Moscow kwamba jeshi lake linaweza kuzilenga meli hizo.

Meli hiyo ya mizigo inayoendeshwa na kampuni ya Ujerumani, ilifanikiwa kupita eneo la Ukraine la Bahari Nyeusi usiku wa jana, masaa kadhaa baada ya kuondoka Odesa. Msemaji wa kampuni hiyo ya Bernhard Schulte Shipmanagement (BSM) amethibitisha hili alipozungumza na shirika la habari la DPA akisema meli hiyo imekwishatoka kwenye eneo la maji la Ukraine.

Soma Zaidi:Droni za Urusi zatishia usalama wa bandari za Danube

Mapema, rais Zelensky alilaani mashambulizi hayo ya Urusi akisema ni kitisho kikubwa kwa usalama wa chakula ulimwenguni, ambayo pia yatachochea ongezeko la gharama za chakula, na pigo dhidi ya utulivu wa kijamii na kisiasa barani Afrika na Asia.

Alisema "Kila shambulizi la Urusi kwenye bandari za Ukraine ni pigo kwenye gharama za vyakula, ni pigo kwa utulivu wa kijamii na kisiasa sio tu Afrika bali pia Asia. Moja ya vitu vya msingi vinavyowapa jamii maisha ya kawaida ni chakula kuwa mezani kwa ajili ya familia zao."

Rais Volodymyr Zelensky amesifu hatua hiyo ya safari ya kwanza ya meli ya mizigo ya kiraia kuptia Bahari Nyeusi.
Ukraine ilibaki kwenye makubaliano ya kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi na kuepeleka kwa mataifa yanayoendelea hususan Afrika na Asia.Picha: president.gov.ua

Katika hatua nyingine jamii ya kimataifa pia imelaani na kuyakosoa mashambulizi hayo ya Urusi. Marekani imesema mashambulizi hayo yanaonyesha kwamba rais Vladimir Putin hakujali chochote kuhusiana na ugavi wa chakula kwenye mataifa yanayoendelea. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Vedant Patel amewaambia waandishi wa habari kwamba hilo halikubaliki na kuitolea mwito Urusi kurejea mara moja kwenye makubaliano ya nafaka.

Tukiachana na suala hili la usafirishaji wa nafaka, rais Zelensky ametangaza jana kwamba Kyiv inazidi kujiimarisha katika kutengeneza droni. Kwenye hotuba yake ya usiku, Zelensky alisisitiza umuhimu wa ndege hizo zisizotumia rubani katika kulilinda taifa hilo dhidi ya uvamizi wa Urusi. Alisema, droni ni macho na ulinzi kwa wanajeshi wa mstari wa mbele. Lakini pia hakuacha kuwaomba tena washirika wake wa kimataifa kumpatia ndege hizo.

Lakini wakati wakiongeza utengenezaji wa droni, msemaji wa kikosi cha anga cha Ukraine Yuriy Ihnat amesema hawataweza kuzitumia ndege za kivita walizopewa na Marekani, chapa F-16 katika majira yanayokuja ya vuli na baridi. Marekani imekwishasema iko tayari kuisaidia Ukraine kuiangusha Urusi, lakini haitaki kujiingiza moja kwa moja kwenye mapigano kati ya Muungano wa kijeshi wa NATO inaouunga mkono dhidi ya Urusi.