1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais wa mpito wa Sri Lanka atangaza hali ya dharura

Sylvia Mwehozi
18 Julai 2022

Rais wa mpito wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe ametangaza hali ya dharura nchini humo hii leo, katikati ya mkwamo wa kisiasa wakati taifa hilo la kusini mwa Asia likijaribu kuteua uongozi mpya.

https://p.dw.com/p/4EGy3
Sri Lanka | Vereidigung Interimspräsident Ranil Wickremesinghe
Picha: Srilankan PM Media office

Wickremesinghe ametangaza hali ya dharura akisema ilikuwa ni muhimu kwa maslahi ya usalama wa umma, kurejesha utulivu na huduma muhimu kwa maisha ya jamii. Tangazo la hali ya dharura limetolewa wakati chama cha wanafunzi wa vyuo vikuu kikiitisha mgomo mkubwa Jumanne, siku ambayo bunge litaitisha kura ya kuchagua rais. Kura hiyo miongoni mwa wabunge 225 imepangwa kufanyika Jumatano.

Wabunge waliokutana siku ya Jumamosi walianza mchakato wa kumchagua kiongozi mpya kuliongoza taifa hilo. Uteuzi kwa ajili ya uchaguzi wa rais mpya utafanyika kesho Jumanne na ikiwa kutakuwa na mgombea zaidi ya mmoja basi wabunge watapiga kura Jumatano.Sri Lanka yatangaza hali ya dharura baada ya rais kukimbia

Kaimu rais Wickremesinghe pia ameliagiza jeshi la polisi kufuatilia mitandao ya kijamii, baada ya ujumbe kadhaa kusambazwa katika mitandao kwamba wabunge watakaokiuka matakwa ya waandamanaji watazuiwa kurejea nyumbani kwao.

Sri Lanka | Vereidigung Interimspräsident Ranil Wickremesinghe
Ranil Wickremesinghe akiapishwa kukaimu nafasi ya uraisPicha: Sri Lankan President's Office/AP Photo/picture alliance

"Hatua za haraka pia zitachukuliwa kulinda sheria na utulivu wa nchi. Ninakiri kwa asilimia 100 juu ya haki ya kuandamana kwa amani. Lakini baadhi ya makundi yamekuwa yakijaribu kujihusisha na hujuma. Pia kumekuwa na ripoti kwamba baadhi ya makundi mengine yanaweza kufanya majaribio ya kushinikiza wabunge katika mchakato wa kuchagua rais mpya," alisema Wickremesinghe.

Wickremesinghe aliapishwa rasmi kuwa kaimu rais siku ya Ijumaana bado pia ni waziri mkuu wa nchi. Kiongozi huyo ni miongoni mwa wagombea wawili wanaoongoza kuchukua wadhifa huo wa urais. Hadi sasa wapo wagombea wanne.

Hata hivyo waandamanaji wamekuwa wakipiga kampeni ya kumpinga Wickremesinghe, wakidai kwamba ni mshirika wa karibu wa rais aliyejiuzulu Gotabaya Rajapaksa na kisha kukimbia nchi. Ulinzi katika eneo la bunge umeimarishwa.

Hali ya dharura iliyotangazwa na Wickremesinghe inahusisha sehemu ya sheria za usalama wa taifa na kumruhusu kiongozi huyo kutunga kanuni kwa maslahi ya usalama wa umma, kurejesha hali ya utulivu, kukabiliana na uasi na ghasia za kiraia au kwa ajili ya matengenezo ya vifa muhimu.

Chini ya kanuni za hali ya dharura, Wickremesinghe anaweza kutoa amri ya kukamatwa, kumiliki mali yoyote na kukagua maeneo yoyote. Vilevile anayo mamlaka ya kubadili au kusimamisha sheria yoyote.

Sri Lanka nchi ya kisiwa yenye wakaazi takribani milioni 22 hivi sasa ipo katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta.

Hadi kufikia siku ya Jumapili, vuguvugu la maandamano ilikuwa imefikia siku ya 100. Maandamano yamepungua kwa kiasi kikubwa tangu Rajapaksa aikimbie nchi na kujiuzulu, lakini baadhi ya watu karibu 500 wameendelea kukalia sehemu ya majengo ya Ikulu ya rais baada ya kuyavamia.