1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi apanga katiba mpya; upinzani wahisi ni njama

25 Oktoba 2024

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, ametangaza mpango wa kuunda kamisheni ya kuchunguza marekebisho ya katiba, ambayo huenda yakatoa ukomo wa mihula na kumwezesha kugombea muhula wa tatu.

https://p.dw.com/p/4mDnb
Felix Tshisekedi katika mahojiano na DW
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi Picha: DW

Tshisekedi aliapishwa madarakani mwezi Januari baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili na wa mwisho mnamo mwezi desemba. Siku ya Jumatano, alitangaza mipango ya kuangalia uwezekano wa kurekebisha katiba, akisema kuwa katiba ya sasa, iliyoridhiwa kupitia kura ya maoni mwaka 2005, haiendani na hali halisi ya sasa ya nchi.

"Katiba yetu si nzuri," Tshisekedi alisema Jumatano wakati wa ziara rasmi mjini Kisangani, mji mkuu wa Jimbo la Tshopo kaskazini mashariki mwa nchi. "Iliandikwa nje ya nchi na wageni," aliongeza, akirejelea makubaliano ya amani ya 2003 yaliyosainiwa Afrika Kusini ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa.

Katiba ya sasa ya Kongo iliandikwa nchini humo na kupitishwa kupitia kura ya maoni mwaka 2006. Hii ni katiba ya sita ya nchi hiyo tangu ilipojipatia uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960. Tshisekedi amekosoa katiba ya sasa mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni, akisema kuwa imepitwa na wakati.

Tshisekedi ameeleza kuwa mchakato wa maamuzi unaochelewa na mvutano kati ya magavana na mabunge ya majimbo ni sababu za kuandaa katiba mpya. Alisema pia kuwa uamuzi wa kubadilisha ukomo wa mihula ya urais ni wa wananchi, si wa rais, lakini hakutoa maelezo kuhusu jinsi wajumbe wa kamisheni watakavyoteuliwa.

Wapinzani wahofia mabadiliko ya ukomo wa mihula

Afrika Goma Wahlkampf Martin Fayulu
Mwanasiasa wa upinzani DRC Martin Fayulu Picha: Benjamin Kasembe/DW

Viongozi wa kisiasa wa upinzani nchini Kongo wanaiona hatua ya Tshisekedi kama mbinu ya kuendeleza muda wake madarakani, ikifanana na hatua kama hizo zilizochukuliwa katika nchi nyingine za Afrika kama Guinea chini ya rais wa zamani Alpha Conde na Cameroon chini ya Rais Paul Biya.

Chama kikuu cha upinzani, Together for the Republic, kililaani tangazo la Tshisekedi. Msemaji wa chama hicho, Hervé Diakiese, alisema ni uongo kudai kuwa katiba iliyopitishwa na raia wa Kongo kupitia kura ya maoni iliandikwa na wageni, akiongeza kuwa serikali hii inatafuta suluhisho za uwongo kwa matatizo halisi.

Kiongozi mwingine wa upinzani Claudel Lubaya alisema kwamba kwa kubadilisha kanuni za uongozi ili kubaki madarakani, serikali ya sasa inajaribu tu kuendeleza uwepo wake kisiasa kwa hasara ya matarajio halali ya wananchi kwa utawala wa haki na uwazi.

Katumbi asema katiba Kongo haitabadiliswa

Moise Katumbi kutoka DR Congo
Kiongozi wa upinzani wa Kongo Moise Katumbi akiwa katika picha wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 23 Machi 2019 mjini Brussels.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Moise Katumbi, kiongozi mwingine wa upinzani na aliyekuwa mshindani wa pili katika uchaguzi wa Desemba, alisema katiba haitabadilishwa kwani ilipitishwa na wananchi wa Kongo, akisisitiza kwamba tatizo la Kongo ni utawala mbovu, si katiba.

Fred Bauma, mwanaharakati wa haki za binadamu na kiongozi wa shirika la haki za kijamii The Struggle for Change, alisema kwamba Tshisekedi aliapa kuheshimu na kulinda katiba wakati wa kuapishwa kwake mapema mwaka huu.

Soma zaidi:Tshisekedi amshutumu Kabila kwa kuunga mkono waasi

"Leo anajitokeza kama mkosoaji mkuu wa katiba, baada ya kuivunja mara kadhaa," aliandika kwenye X. Wataalamu wanasema Tshisekedi ana uwezo wa kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba, lakini itabidi idhinishwe na asilimia 60 ya wabunge au kupitishwa kwa kura ya maoni na zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura.