1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto awatimua mawaziri, mwanasheria mkuu Kenya

11 Julai 2024

Rais wa Kenya William Ruto amewafuta kazi mawaziri wake wote nan kuahidi kuunda serikali mpya ambayo itakuwa ndogo na yenye ufanisi kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kupinga kodi kubwa na utawala mbaya.

https://p.dw.com/p/4iBm8
Kenia Nairobi | Rais wa Kenya William Ruto
Rais William Ruto amesema ataunda baraza jumuishi na lenye ufanisi baada ya kuvunja baraza la sasa.Picha: TONY KARUMBA/AFP

Ruto alisema alichukua uamuzi huo baada ya kuwasikiliza wananchi na kwamba ataunda serikali pana baada ya mashauriano. Kenya imeshuhudia machafuko ya wiki tatu ambapo waandamanaji walivamia bunge tarehe 25 Juni baada ya mswada wa fedha kupitishwa unaopendekeza nyongeza ya kodi. Zaidi ya watu 30 walikufa katika maandamano hayo, ambayo yamebadilika na kuwa shinikizo la kumtaka rais ajiuzulu.

Ruto alisema Waziri kiongozi, Musalia Mudavadi, mshirika muhimu wa kisiasa, atasalia ofisini.

Soma pia: Ruto: "Sina hatia" na vifo vya waandamanaji

Alisema uamuzi wa kuvunja baraza la mawaziri umefuatia "tathmini ya kina ya utendaji" wa Baraza la Mawaziri na kwamba serikali mpya itamsaidia "kuharakisha utekelezaji wa lazima, wa haraka na usioweza kutenduliwa wa mipango muhimu ya kushughulikia mzigo wa deni, kuinua rasilimali za ndani, kuongeza nafasi za kazi, kuondoa ubadhirifu na kupunguza wingi wa mashirika ya serikali na kuua joka la ufisadi."

Ruto aliteua mawaziri 21 baada ya kuchaguliwa kwake mwaka wa 2022. Wakosoaji walimshutumu rais kwa kuchagua washirika wake wa kisiasa na kuachana na desturi ya awali ya kuchagua wataalamu kusimamia wizara.

Nairobi Kenya | Maandamano ya kupunga sheria ya fedha 2024.
Maandaano ya vijana maarufu Gen Z yamemlaazimu Rais Ruto kubadili msimamo kuhusu mambo mengi na hatimaye kulivunja baraza lake la mawaziri.Picha: James Wakibia/Sipa USA/picture alliance

Mawaziri watatu walijiuzulu nyadhifa zao za kuchaguliwa ili kuchukua nyadhifa za uteuzi wa uwaziri. Wengine walishindwa katika uchaguzi na walionekana kuwa walitunukiwa uteuzi wa kisiasa na rais. Wizara kadhaa zikiwemo za kilimo na afya zimegubikwa na kashfa za rushwa zinazohusisha mbolea feki na matumizi mabaya ya fedha.

Soma pia: Rais William Ruto wa Kenya aahidi mabadiliko baada ya maandamano

Waandamanaji walilishutumu Baraza la Mawaziri kwa kutokuwa na uwezo, kiburi na kujionyesha kwa utajiri huku Wakenya wakikabiliana na ushuru mkubwa na gharama kubwa za maisha.

Waandamanaji walimtaka rais ajiuzulu licha ya kubali uamuzi wake wa kusaini mswada wa sheria ya fedha uliopendekeza ushuru wa juu. Ruto mnamo Ijumaa aliomba radhi kwa "kiburi" cha wabunge na mawaziri na kusema aliwajibika na atazungumza nao.

Pia alitangaza hatua za kubana matumizi ikiwa ni pamoja na kuvunjwa kwa mashirika 47 ya serikali na shughuli zinazoingiliana ili kuokoa pesa na kuondoa bajeti ya ofisi ya mke wa rais, miongoni mwa nyingine.

Mchambuzi siasa Herman Manyora ametaja kutimuliwa kwa Baraza la Mawaziri kuwa "hatua ya ujasiri" ambayo ilikuwa muhimu kuzima ghadhabu za raia.

Soma pia: Ruto auondoa kabisa muswada wa fedha 2024

Rais William Ruto avunja baraza lake la mawaziri

Hii ni mara ya kwanza kwa rais aliyeko madarakani kuwafuta kazi mawaziri chini ya katiba mpya. Mara ya mwisho hatua kama hiyo ilitokea mwaka 2005 baada ya kura ya maoni iliyofeli wakati Rais wa wakati huo Mwai Kibaki alipowafuta kazi mawaziri wake ili kurejesha mamlaka yake ya kisiasa.