1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Rais wa Iran alaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Houthi

15 Januari 2024

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, amelaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani nchini Yemen akisema yamefichua kile amekiita kuwa "tabia halisi" ya Washington ya kuendekeza shari.

https://p.dw.com/p/4bEfh
Mfereji wa Suez kwenye Bahari Nyekundu
Ujia wa mfereji wa Suez kwenye Bahari Nyekundu Picha: Sayed Hassan/dpa

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Iran, IRNA, likinukuu mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Raisi na kiongozi mkuu wa waasi wa Houthi wa nchini Yemen, Mahdi al-mashat.

Akizungumzia mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za Wahouthi nchini Yemen, Raisi amesema hayo ni matendo "yanayopingwa na kulaaniwa na nchi zote zinayopendelea uhuru duniani."

Washington imekuwa ikizilenga ngome za waasi Houthi kwa kile viongozi wa Marekani wanasema kurejesha usalama kwenye njia muhimu ya biashara kwenye Bahari Nyekundu.

Waasi hao wamekuwa wakizilenga meli za mizigo kwa makombora na droni kwa lengo la kuishinikiza Israel isitishe kampeni ya kijeshi huko Gaza.

Kiongozi wa Iran amemweleza Al-Mashat kwamba kuwaunga mkono Wapalestina "wasio na nguvu" ni msimamo usioyumba wa Iran.