1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Guinea-Bissau anusurika jaribio la mapinduzi

2 Februari 2022

Rais wa Guinea-Bissau ametangaza kuwa amenusurika katika jaribio la mapinduzi ambalo limesababisha vifo vya watu wengi na kusema kwa sasa hali imedhibitiwa.

https://p.dw.com/p/46PL9
Guinea -Bissau | Präsident Umaro Sissoco Embalo hält eine Pessekonferenz
Rais wa Umaro Sissoco Embalo asema hali kwa sasa imedhibitiwa nchini humo Picha: Aliu Balde/Xinhua/picture alliance

Rais wa nchi hiyo Umaro Sissoco Embalo amewaambia waandishi wa habari kwamba alikabiliwa na milio ya risasi na silaha nzito kwa takriban saa tano akiwa na mshauri wa kijeshi, waziri na walinzi wawili katika mji mkuu Bissau wakati wa njama ya kumuua rais wa jamhuri na baraza zima la mawaziri.

Rais Umaro amesema Washambuliaji wangeweza kuzungumza naye kabla ya matukio haya ya umwagaji damu ambayo yamesababisha vifo na majeruhi.

Guinea-Bissau inayokabiliwa na mapinduzi inapambana na sifa ya vitendo vya rushwa na magendo ya madawa ya kulevya na rais aligusia hili bila kuwataja waliojaribu kuipindua serikali yake. Akionekana mtulivu, amesema  kuwa tukio hilo lililoshindwa linahusishwa na maamuzi aliyochukua, hasa ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na ufisadi.

Guinea-Bissau | Unruhen | Soldaten in Bissau
Ulinzi umeimarishwa katika mitaa ya BissauPicha: AFPTV teams/AFP/Getty Images

"Sio askari pekee waliohusika, lakini zaidi ni vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ndiyo iliyosababisha, watu wengi waliohusika wapo kwenye orodha ya watu wanaochunguzwa na biashara ya dawa za kulevya, nina wazo la kiasi gani watalazimika kulipia hili. Ninaweza kuwaahidi kwamba mapambano yataendelea."

Siku ya Jumanne mchana, watu waliokuwa na silaha nzito nzito walizingira majengo ya serikali, ambako Rais Embalo na Waziri Mkuu Nuno Gomes Nabiam waliaminika kuwa walikuwa wakihudhuria mkutano wa baraza la mawaziri.

Watu walionekana wakikimbia eneo hilo kwenye ukingo wa Bissau, karibu na uwanja wa ndege. Masoko ya eneo hilo  na benki yalifungwa huku magari ya kijeshi yaliyojaa askari yakiranda mitaani. 

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alielezea wasiwasi wake juu ya jaribio hilo la mapinduzi huku Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ikitoa taarifa ya kulaani jaribio hilo la mapinduzi na kuwataka wanajeshi kurejea kwenye ngome zao.

Guinea-Bissau ni koloni la zamani la Ureno na jimbo maskini la pwani lenye takriban watu milioni mbili lililo kusini mwa Senegal. Nchi hiyo imeshuhudia misururu minne ya mapinduzi ya kijeshi tangu kupata uhuru wake mwaka 1974, na tukio la hivi karibuni ni la mwaka 2012.

Nchi hiyo ambayo jeshi lina ushawishi mkubwa, iliapa kurejea katika demokrasia mwaka 2014, lakini imekuwa na utulivu mdogo tangu wakati huo.

afp, ap, reuters, dpa