1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Burkina Faso azuiliwa na majeshi

24 Januari 2022

Duru za kiusalama na mwanadiplomasia mmoja Afrika Magharibi wanasema majeshi yanamzuia Rais wa Burkina Faso Roch Kabore katika kambi ya jeshi kufuatia ufyatuaji wa risasi karibu na makao yake mjini Ouagadougou.

https://p.dw.com/p/45zun
Schwere Schusswechsel in mehreren Kasernen in Burkina Faso
Picha: Sophie Garcia/AP/dpa/picture alliance

Jumatatu asubuhi, magari kadhaa ya kijeshi ambayo kawaida huwa katika msafara wa rais yameonekana karibu na ikulu yakiwa na alama za risasi huku gari moja likiwa na damu. Wakaazi wanaoishi karibu na rais wameripoti ufyatuaji mkali wa risasi usiku kucha.

Kwa sasa haijulikani alipo Kabore wala hali yake ikoje huku kukiwa na ripoti zinazokinzana kutoka kwa duru za kiusalama na kidiplomasia.

Burkina Faso Ouagadougou Unruhen
Majeshi wakiwa nje ya mojawapo ya kambi za kijeshi katika Mji Mkuu OuagadougouPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Amri ya kutotoka nje yatolewa na shule zafungwa

Hapo Jumapili usiku serikali ilikanusha kwamba kulikuwa na mapinduzi kwani milio ya risasi ilisikika kwa wingi kutoka kambi kadhaa za kijeshi huku wanajeshi wanaoongoza mapinduzi hayo wakitaka uungwaji mkono zaidi kutoka kwa serikali katika makabiliano yao na wanamgambo wa Kiislamu.

Rais Kabore Jumapili alitoa amri ya watu kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na moja na nusu alfajiri. Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ya ECOWAS imetoa taarifa ya kumuunga mkono Kabore ambaye kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akilengwa na maandamano ya kumtaka aachie ngazi.

Marufuku hiyo ya kutotoka nje haijulikani itaisha lini ila shule nchini humo pia zimefungwa kwa kipindi cha siku mbili.

Katika miezi ya hivi karibuni raia wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi wameghadhabishwa na hatua ya wanamgambo kuwauwa mara kwa mara raia na wanajeshi. Baadhi ya wanamgambo hao wanadaiwa kuwa na mafungamano na makundi ya kigaidi ya Dola la Kiislamu na al Qaeda.

Hapo Jumapili waandamanaji walijitokeza kuwaunga mkono wanajeshi waliokuwa wanafanya mapinduzi na wakavamia makao makuu ya chama cha kisiasa cha Kabore.

Mapinduzi nchi kadhaa Afrika Magharibi katika miezi 18 

Mchambuzi wa masuala ya kiusalama Mahamoudou Sawadogo baada ya kuulizwa na mwandishi wa DW mjini Ouagadougou Richard Tiene kuhusiana na hali hiyo inayoendelea nchini humo, amesema,

"Kihistoria majeshi ndiyo kama ukuta wa mwisho wa hali mbaya inayoanzishwa na wanasiasa. Nafikiri tunastahili kujifunza kutokana na yote haya na yale yaliyotokea nchini Guinea na Mali ili tusiwe na matatizo kama hayo," alisema Sawadogo.

Hali hii ya Burkina Faso inakuja baada ya mapinduzi nchini Mali na Guinea katika kipindi cha miezi 18 iliyopita ambapo jeshi lilimuondoa madarakani rais Alpha Conde Septemba 2021.

Burkina Faso Unruhen
Majeshi yafyatua mabomu ya kutoa machozi kuawatawanya waandamanajiPicha: Sophie Garcia/AP Photo/picture alliance

Nchini Chad pia, jeshi lilichukua madaraka baada ya Rais Idriss Deby kufariki dunia katika uwanja wa mapigano.

Burkina Faso ni mojawapo ya nchi maskini Afrika Magharibi licha ya kuwa na madini ya dhahabu. Jeshi lake limepata hasara kubwa mikononi mwa wanamgambo ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo na wamewalazimisha raia katika maeneo waliyoko kufuata sheria zao kali za Kiislamu.

Vyanzo: Reuters/DPAE