1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Vladimir Putin ayasifia mahusiano yake na Xi Jinping

15 Septemba 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping wamekutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine, wakisifu ushirikiano wao wa kimkakati dhidi ya Mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/4Gw1r
Wladimir Putin  Xi Jinping in Samarkand Usbekistan
Picha: SPUTNIK via REUTERS

Viongozi hao walikutana pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai SCO , katika taifa la zamani la muungano wa kisovieti la Uzbekistan. Mkutano huu ni sehemu ya ziara ya Xi nje ya nchi tangu kuanza kwa Janga la Corona, na kwa Putin mkutano huu ni nafasi ya kuonyesha Urusi haijatengwa kikamilifu licha ya juhudi za Mataifa ya Magharibi kutaka hilo lifanyike kutokana na hatua yake ya kuivamia Ukraine.

Xi alimuambiwa Putin kwamba taifa lake liko tayari kuweka juhudi tofauti na Urusi kuchukua jukumu la kuwa mataifa yaliyo na nguvu zaidi na kuwa na jukumu pia la kuongoza  ili kuchangia uthabiti na utulivu katika dunia inayotikiswa na migogoro ya kijamii. Putin pia aliigusa Marekani moja kwa moja ambayo imekuwa ikiongoza juhudi za kuiunga mkono Ukraine na kuiwekea vikwazo Urusi, akisema jaribio la taifa hilo kutaka ulimwengu unaoendeshwa na dola moja limefeli na ni jambo lisilokubalika.

Kiongozi huyo wa Moscow amesifia pia msimamo wa kati uliochukuliwa na China katika mzozo wa Urusi na Ukraine huku akisisitiza kuwa taifa lake linaiunga mkono China katika mzozo wake na Taiwan akisema anaheshimu kanuni ya China moja akikosoa kile alichokiita uchokozi wa Marekani wa kuipa Taiwan usaidizi wa kijeshi wa mabilioni ya dola.

Kremlin imesema kuna njia mbadala kando na uwepo wa taasisi zinazotawaliwa na Magharibi

Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin Poo//AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Kulingana na Ikulu ya Urusi mkutano wa SCO mjini Samarkand unaonesha kuwa kuna njia mbadala kando na uwepo wa taasisi zinazotawaliwa na Magharibi. Jumuiya ya SCO inayujumuisha China, Urusi, India, Pakistan na mataifa manne ya Asia ya Kati ambayo ni Kazakhstan, Kyrgyzstan, Uzbekistan na Tajikistan, iliundwa mwaka 2001 kama shirika la kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa taasisi hasimu za Marekani.

Viongozi wa Mataifa wanachama wa SCO watahudhuria mkutano huo wa leo na kesho utakaohudhuriwa pia na rais wa Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Mapema leo alhamisi Putin alikutana na viongozi wa Kyrgyzstan naTurkmenistan, rais Raisi na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.

Soma zaidi: Xi na Putin kukutana katika mkutano wa SCO, Uzbekistan

Amesema Ushirikiano na mataifa hayo unaendeleo vizuri. Kwa upande wake rais wa Iran amemuhakikishia Putin kwamba uhusiano wao utaimarika zaidi hasa kutokana na mataifa yote kuwekewa vikwazo na Marekani. Raisi amesema Marekani inafikra mbaya ya kutarajia kulikwamisha taifa inaloliwekea vikwazo...amesema ni wakati wa kuzipuzilia mbali fikra kama hizo.

Chanzo: afp,dpa