1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Steimeier achaguliwa kwa muhula wa pili

14 Februari 2022

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amechaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mitano jana Jumapili, baada ya mkutano maalum wa wabunge 736 na wawakilishi wa majimbo 16 ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/46z2p
Deutschland | Bundesversammlung | Bundespräsident Steinmeier wiedergewählt
Picha: Jens Schlueter/AFP

Steinmeier anaoneka kama ishara ya makubaliano na ameapa kuponya majeraha yaliyoachwa na janga la corona na kuahidi kupigana na maadui wa demokrasia.

Mwanasiasa huyo mahiri mwenye umri wa miaka 66 wa chama cha Social Democratic (SPD) aliungwa mkono na vyama vyote vitatu vinavyounda serikali ya mseto pamoja na chama cha upinzani cha wahafidhina cha Christian Democratic Union (CDU).

soma Rais Steinmeier aungwa mkono na chama kikuu cha upinzani

Demokrasia dhabiti

Deutschland | Bundesversammlung | Bundespräsident Steinmeier wiedergewählt
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Steinmeier katika hotuba kwenye Bunge Maalum baada ya kukubali kuchaguliwa kwake, amesema wajibu wake ni kuwatumikia watu wote wa Ujerumani na amesisitiza kuwa haegemei upande wowote.

"Bi rais wa Bunge, wajumbe wapendwa, nawashukuru. Nashukuru kwa imani ya walionipigia kura na ninaomba imani kwa wale ambao hawakuweza kufanya hivyo leo. Ofisi ya Rais wa Shirikisho si ya upendeleo na ninawaahidi ndivyo nitakavyoiendeleza. Wajibu wangu ni kwa watu wote wanaoishi katika nchi yetu. Kwa hiyo, bila upendeleo wa chama nitakuwa ndiyo, lakini siegemei upande wowote linapokuja suala la demokrasia. Yeyote anayepigania demokrasia mimi niko upande wake, yeyote atakayeishambulia atakuwa mpinzani wangu."

soma Steinmeier ahimiza mshikamano kwa wajerumani

Katika kukabiliana na mgogoro unaoongezeka kwenye mpaka wa Ukraine ambapo Urusi imekusanya zaidi ya wanajeshi 100,000, Steinmeier alionya kwamba Ulaya iko katikati ya hatari ya mzozo wa kijeshi na iwapo vita vitatokea katika Ulaya Mashariki, Urusi inawajibika kwa hilo.

Steinmeier ameapa kwamba ataendelea kufanyia kazi kuimarisha demokrasia nchini Ujerumani na kusaidia kuondoa hofu ya baadaye na kuwapa raia wa nchi hiyo ujasiri wa kushughulikia changamoto katika siku za mbeleni.

Kiungo muhimu katika siasa za Ujerumani

Deutschland | Schloss Bellevue - Ernennungsurkunde Scholz
Kansela Ujerumani Olaf Scholz na Rais Frank-Walter SteinmeierPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alimpongeza Steinmeier, akisema kwamba ameonyesha kuwa yuko katika nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na watu, kuhakikisha mshikamano katika jamii, lakini pia kutoa mwongozo.

Scholz ameongeza kuwa kutokana na weledi wa Steinmeier katika siasa za Ujerumani ni kiongozi muhimu hasa wakati huu ambapo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo janga la corona lakini pia kuhusu kulinda amani barani Ulaya akisema kwamba Steinmeier ni rais sahihi katika wakati sahihi kabisa.

soma Steinmeier ahimiza ushirikiano wa kimataifa

Wadhifa wa rais nchini Ujerumani ni wa heshima tu na rais ana uwezo mdogo wa kiutendaji lakini anazingatiwa kuwa na mamlaka muhimu ya kimaadili. Mnamo mwaka 2017 baada ya uchaguzi uliokuwa na utata wa bunge, Rais Steinmeier alisaidia kuwachochea wanasiasa kuunda serikali mpya ya muungano badala ya kushikilia uchaguzi mpya.

Wagombea wengine watatu waligombea ofisi hiyo ya juu zaidi nchini Ujerumani ingawa hawakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

 

Vyanzo/Reuters/AP/dpa