1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia: Matumizi ya kuni na mkaa chanzo cha ukame

1 Novemba 2022

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika mjadala wa kitaifa wa kutafuta suluhu ya nishati safi ya kupikia na amesema hatua ya kwanza kuelekea suluhisho ni Watanzania wenyewe kubadilisha mtazamo wao.

https://p.dw.com/p/4Iusb
Samia Hassan | Präsidentin von Tansania
Picha: Hannah Mckay/AFP/Getty Images

Taarifa zilizotolewa katika mjadala huo wa kitaifa, zimeeleza kuwa Watanzania wanaotumia nishati safi ni asilimia tano tu, na waliobaki wakitumia kuni na mkaa, hali iliyotajwa kuwa ndicho chanzo cha vifo takribani 33,000 kila mwaka nchini.

Ni mjadala unaowaleta pamoja wadau mbalimbali wa afya, nishati, mazingira, uwekezaji na watunga sera, kubadilishana mawazo juu ya namna Tanzania itakavyopambana na changamoto ya matumizi ya nishati chafu, na kuingia katika matumizi ya nishati safi.

Watanzania wabadili mtazamo

Akizungumza wakati akizindua mjadala huo wa kitaifa wa siku mbili, Rais samia amesema suluhisho muafaka katika kupambana na matumizi ya kuni na mkaa, kwanza ni kwa Watanzania wenyewe kubadili mitazamo.

Kadhalika, Rais Samia amesema matumizi ya kuni na mkaa ni suala mtambuka nchini Tanzania, kwani ndicho chanzo cha ukame unaosababisha uhaba wa maji, chanzo cha magonjwa na ndicho chanzo cha unyanyasaji wa kijinsia.

Kongo Holzkohleproduktion bedroht zweitgrößten Regenwald der Welt
Wanawake wakiwa wanauza mkaa kwa matumizi ya kupikiaPicha: Jonas Gerding/DW

Aidha, aliyewahi kuwa mbunge na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameshiriki mjadala huo na kuitaka kwanza serikali ibadili sera na kuwataka wafanyabiashara kuangalia suala la bei katika nishati mbadala.

Wanamazingira wapambane na matumizi ya nishati chafu 

Profesa Tibaijuka amesema mijadala hii iwe endelevu ili Watanzania na wadau wengine wa mazingira wajue namna ya kupambana na matumizi ya nishati chafu ambayo amesema ina madhara mengi wakati Watanzania wengi wakiwa na uelewa mdogo kuhusu tatizo hilo.

Mtu mwingine aliyechangia hoja ni mtalaam mwandamizi wa masuala ya fedha wa Shirika la Umoja wa Mataifa Mitaji ya Maendeleo, Emmanuel Muro, ambaye amesema asilimia hamsini na mkaa unaotumika Dar es Salaam, unatoka katika mikoa mitano ambayo ndiyo chanzo cha maji.

Zaidi ya wadau 3,000 wameshiriki mjadala huo wa kihistoria wa kutafuta suluhu ya nishati chafu ya kupikia nchini Tanzania, mjadala ulioongozwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba.