1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia akutana na Rais Ndayishimiye Bujumbura

Amida Issa16 Julai 2021

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan yuko katika ziara ya siku mbili nchini Burundi. Tayari amefanya mazungmzo na mwenyeji wake Rais Evariste Ndayishimiye.

https://p.dw.com/p/3wac3
Burundi Bujumbura | Evariste Ndayishimiye, Präsident & Samia Suluhu Hassan, Präsidentin
Picha: Bujumbura Amida Issa/DW

Viongozi hao wamekubaliana kukuza ushirikiano baina ya nchi zao katika sekta mbali mbali mbali. Rais Samia ameahidi kuwa Tanzania itaendeleza juhudi zake kuhakikisha Burundi inaondolewa vikwazo vyote ilivyowekewa na jumuiya ya kimataifa. 

Kwenye uwanja wa kimataifa wa Bujumbura rais wa Tanzania Bi. Samia Suluhu Hassan alilakiwa na Makamu wa Rais Prosper Bazombanza na mawaziri kadhaa wa serikali, huku raia wa kawaida wakimpokea kwa nyimbo na nderemo.

oma pia: Rais Ndayishimiye awakaribisha wawekezaji Burundi

Baada ya hapo Rais Samia alielekea ikulu na kupokelewa kwa heshima na mizinga 21 ya jeshi.

Kisha alikutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye. Katika mazungumzo yao yaliyodumu muda usiozidi saa 1, viongozi hao wawili walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbali mbali.

Burundi Bujumbura | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania
Picha: Bujumbura Amida Issa/DW

Rais Ndayishimiye ametoa shukran kwa Tanzania kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Burundi huku akisema wamekubaliana kushirikiana kuzuwia kuenea kwa silaha ndogo ndogo katika nchi hizi mbili.

Soma pia: Tanzania na Burundi zajadili kuukabili uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari, rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara yake imedhamiria kukuza uhusiano wa kidugu wa enzi na enzi.

Rais Samia pia ameahidi  kuwa Tanzania itaendelea kupaaza sauti ili vikwazo Burundi ilowekewa na jamii ya kimataifa viondolewe.

Rais huyo wa Tanzania amesema uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili umejikita zaidi kwenye maswala ya kiuchumi na kibiashara. Hivyo wameangazia jinsi ya kukuza uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi
Rais Evariste Ndayishimiye wa BurundiPicha: Bujumbura Amida Issa/DW

Pia wamekubaliana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuondoa vikwazo vya kodi na visivyo vya kodi. Ujenzi wa kituo cha huduma za pamoja utaharakishwa kwenye eneo la mpakani la Manyovu Mugina.

Rais Samia amesema wameangazia pia sekta ya madini na kuelezea kwamba Burundi, ina hazina kubwa ya madini ya Nickel na Chuma katika mkoa wa Rutana, madini hayo yanapatikana pia Kabanga Tanzania. Hivyo watashirikiana katika uchimbaji na kutafuta soka la madini hayo.

Tayari Rais Samia amezuru Kiwanda cha Fomi kinachotengeneza mbolea za kisasa na ataitembelea Benki ya Tanzania CRDB tawi lake la Burundi, kabla ya jioni hii kukirimiwa kwa chakula cha jioni na mwenyeji wake rais Ndayishimiye.

Amida ISSA