1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia aagiza hatua za haraka kusaidia wahanga wa mafuriko

Veronica Natalis
4 Desemba 2023

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameziagiza mamlaka nchini humo kuelekeza nguvu za uokozi na utafiti kwenye eneo la Katesh baada ya mafuriko kusababisha vifo vya watu wapatao 50 kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4Zk5w
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametangaza hatua maalum za kukabili athari za mafuriko yaliyouwa takribani watu 50 kaskazini mwa nchi yake.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametangaza hatua maalum za kukabili athari za mafuriko yaliyouwa takribani watu 50 kaskazini mwa nchi yake.Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Vifo vya watu hao pamoja na majeruhi zaidi ya 80 vilitokana na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Jumapili (Disemba 3) na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo kutoka milimani.

Akiwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaofanyika mjini Dubai, Rais Samia alisema amesikitishwa na vifo hivyo na kuagiza "nguvu kubwa ya serikali ielekezwe katika wilaya ya Hanang ili kuwasaidia." wananchi. 

Kulingana na mamlaka za serikali nchini Tanzania, mvua kubwa zilianza kunyesha majira ya saa 11:00 alfajiri ya Jumapili na zikasababisha mafuriko yaliyoporomosha tope kutoka Mlima Hanang, mlima wa Volkano ulio na urefu wa mita 3,418 juu ya usawa wa bahari.

Mafuriko yauwa watu karibu 50 Tanzania

Vifo zaidi viliripotiwa kutokea katika maeneo ya Katesh na Gendabi katika wilaya hiyo ya Hanang, maeneo ambayo yapo karibu na mlima huo.

Mashahidi walioshuhudia maafa hayo waliiambia DW kwamba "watu wengine waliopoteza maisha walisombwa na mafuriko ya mkondo wa maji.

Uwezekano wa vifo kuongezeka

Serikali mkoani Manyara ilisema kulikuwa na uwezekano idadi hiyo kuongezeka kwa sababu juhudi za kutafuta miili mingine zilikuwa bado zinaendelea.

Hali baada ya mafuriko na maporomoko yaliyouwa watu wapatao 50 eneo la Katesh kaskazini mwa Tanzania.
Hali baada ya mafuriko na maporomoko yaliyouwa watu wapatao 50 eneo la Katesh kaskazini mwa Tanzania.Picha: Xinhua/picture alliance

Wakati majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali na vituo vya afya na wanaopata nafuu wanaruhusiwa kutoka, baadhi ya familia zilikuwa zimeripoti kutokuwaona ndugu zao zaidi ya masaa 24 baada ya mafuriko na maporomoko hayo.

Soma zaidi: Takriban watu 47 wamekufa Tanzania kufuatia maporomoko ya ardhi

Mbali na vifo na majeruhi, kumeripotiwa pia uharibufu wa makaazi, vyombo vya usafiri pamoja na miundombinu ya barabara.

Hadi DW inamaliza kukusanya taarifa hii, hakukuwa na na tathmini rasmi iliyotolewa na serikali ingawa kulingana na mkuu wa mkoa huo, Qeen Sendiga, kikosi cha kupambana na maafa chini ya ofisi ya waziri mkuu tayari kilishawawili kwenye eneo la tukio kwa ajili ya uokozi na tathmini.