Rais Obama akutana na viongozi vijana wa Afrika
4 Agosti 2010Rais Barack Obama wa Marekani amewatolea wito viongozi vijana wa bara la Afrika kufanya mabadiliko kwa ajili ya bara hilo na kudumisha demokrasia, huku akiwatupia lawama viongozi wengi walioingia madarakani baada ya mataifa yao kupata uhuru ambao wanang'ang'ania kubakia madarakani. Rais Obama aliutoa wito huo jana alipokutana na zaidi ya viongozi vijana 100 wa bara la Afrika katika Ikulu ya Marekani katika kongamano la kuadhimisha miaka 50 tangu mataifa mengi ya Afrika yalipopata uhuru wao mwaka 1960. Rais Obama aliwaambia vijana hao kuwa siku moja baadhi yao watakuwa viongozi wa mataifa yao. Kiongozi huyo wa Marekani alisema katika miaka ya 1960 wakati bibi na babu wa vijana hao wakipigania uhuru, viongozi wa mwanzo wote walisema wanapigania demokrasia. Aidha, Rais Obama ambaye ni Muamerika Mweusi wa kwanza kuiongoza Marekani, alisifu jitihada za viongozi wa Afrika za kutaka kujitawala wenyewe, jambo lililosaidia bara hilo kuepukana na ukoloni.
Anasema lakini kinachotokea hivi sasa ni kwamba kiongozi akikaa madarakani kwa muda anataka kuwa mtawala mzuri na kudai kuwa hiyo ni kwa maslahi ya watu wake, jambo linalosababisha kiongozi huyo kubadilisha sheria za nchi na kuanza kuwatisha na kuwafunga wapinzani wake. Rais Obama aliwatahadharisha viongozi hao vijana kuwa muda si mrefu wao pia wakiingia madarakani watatoa ahadi nyingi nzuri zenye matumaini kwa wananchi wao, lakini mwisho wa siku wanakuwa kama viongozi ambao wao wenyewe walikuwa wakiwapinga. Akitumia maneno ya Mahatma Ghandi, Rais Obama alisema, nanukuu: ''Moja ya vitu ambavyo kila mtu hapa anapaswa kufanya kwa ajili ya maslahi ya taifa, ni wewe mwenyewe unatakiwa konyesha mabadiliko ya hicho kitu unachokitafuta,'' mwisho wa kunukuu. Rais Obama alisema siyo kwamba kila mmoja yuko sawa, kwa sababu kila mtu ana matatizo yake pia, lakini kinachotakiwa ni kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kutumia njia ya amani kwa kuzingatia demokrasia, kitu ambacho kila siku kinapigiwa makelele, na siyo kwa kutumia njia ya umwagaji damu.
Wito wa Clinton kwa viongozi hao vijana
Mapema jana, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliwataka vijana hao viongozi wa bara la Afrika kuwawezesha watu wa kawaida na kuongeza kuwa teknolojia ya habari itazizuia serikali zinazoonea wananchi. Bibi Clinton alisema kuwa katika dunia ya sasa viongozi wanaohitajika ni wale watakaoweza kuwawezesha raia wao. Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema anatumai kuwa mataifa ya Afrika yanaweza kusonga mbele kuelekea katika serikali zinazotumia mfumo wa elektroniki kuendesha shughuli zake za kiserikali. Kongamano hilo la siku tatu linawajumuisha viongozi vijana ambao ni waandishi habari, wanaharakati wa haki na demokrasia na wafanyabiashara. Miongoni mwa viongozi wanaohudhuria kongamano hilo ni kutoka taasisi ya mfumo wa uchaguzi na demokrasia ya Angola, Baraza la vijana la taifa la Cameroon na Mradi wa vijana wa demokrasia kutoka Zimbabwe. Wengine ni Shirika la Zen la Chad, Shirika la simu la MTN la Congo, shirika la Eco-Tours la Rwanda na shirika la fedha la Senegal.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)
Mhariri: Miraji Othman