1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf awaonya wanamgambo kusalimu amri au kuuwawa

Mohamed Dahman8 Julai 2007

Uwezekano wa kushambuliwa kikamilifu kwa msikiti uliozingirwa na wanajeshi mjini Islamabad Pakistan umezidi kuwa mkubwa leo hii baada wanamgambo waliojichimbia ndani kumuuwa kwa kumpiga risasi komandoo mwandamizi wakati kikosi maalum cha Pakistan kilipokuwa kikitobowa ukuta kuwasaidia wanawake na watoto kukimbia kutoka eneo hilo.

https://p.dw.com/p/CHBM
Wanajeshi wa Pakistan wakiuzingira msikiti wa Lal Masjid au Msikiti Mwekundu mjini Islamabad.
Wanajeshi wa Pakistan wakiuzingira msikiti wa Lal Masjid au Msikiti Mwekundu mjini Islamabad.Picha: AP

Wanajeshi na magari ya deraya yameuzingira msikiti huo wa La Masjid au Msikiti Mwekundu tokea Jumanne wakati mapambano yalipozuka kati ya wanafunzi wa itikadi kali wenye silaha na wanajeshi wa serikali.

Serikali na maafisa wa kijeshi wanasema sheikh mwanamapinduzi Abdul Rashid Ghazi na wanamgambo kichwa mchungu 50 hadi 60 kutoka makundi ya Pakistan yenye mafungamano na kundi la Al Qaeda wanaongoza mapambano hayo.

Rais Pervez Musharraf hapo jana ametowa onyo kali na kufuta kabisa uwezakano wa serikali kufikia muafaka na wanamgambo hao.

(O-Ton Musharraf)

Musharraf anasema anawaomba watu hao watoke nje na kusalimu amri na kwamba anayasema hayo hapo kuwa iwapo hawatasalimu amri watauwawa.Amesema kuna wanawake na watoto ndani ya msikiti huo na wamekuwa waangalifu tu kuepuka maafa yoyote kwa watu hao.

Sheikh Ghazi amejibu onyo hilo la Musharraf kwa kusema kwamba angelipendelea kufa shahidi.Katika taarifa iliochapishwa na magazeti ya Jumapili sheikh huyo amesema yeye na wafuasi wake wanatumai vifo vyao vitachochea mapinduzi ya Kiislam nchini Pakistan.

Pia anadai kwamba wanafunzi zaidi ya 300 wakiwemo wasichana wameuwawa kwenye operesheni iliofanyika alfajiri leo hii na kwamba marehemu hao wamezikwa kwenye uwa wa msikiti huo.

Serikali inakanusha na kusema kwamba watu 19 tu ndio waliouwawa kutokana na mzozo huo na kwamba sheikh huyo na wafuasi wake wamekuwa wakiwashikilia watu hao mateka na kuwafanya kuwa ngao dhidi ya mashambulizi.