1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Somalia aapa kukabiliana na ugaidi

Sylvia Mwehozi
10 Juni 2022

Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, ameapa kukabiliana na ugaidi katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo, huku pia akiiomba jumuiya ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo dhidi ya kitisho cha njaa.

https://p.dw.com/p/4CVLG
Somalia Präsident Hassan Sheikh Mohamud
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Rais Mohamud ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuapishwa kwake iliyofanyika Alhamis na kuahidi kuibadilisha Somalia kuwa "nchi ya amani" na kurekebisha uharibifu uliosababishwa na migogoro ya kisiasa ya miezi kadhaa. Aidha, kiongozi huyo mpya pia ameahidi kuimarisha sheria na utulivu na kukuza maridhiano. Mohamud ambaye amewahi kuwa rais wa Somalia kati ya mwaka 2012 na 2017, amekuwa rais wa kwanza kushinda muhula wa pili madarakani.

"Tunahitaji kuungana na dunia nzima juu ya usalama na hasa na nchi za Pembe ya Afrika ambazo leo zinakabiliwa na changamoto za kiusalama zinazotokana na makundi ya kigaidi kama al-Shabab, na ISIS."

Somalia | Menschen leiden unter der Dürre
Maelfu ya raia wa Somalia wanakabiliwa na kitisho cha njaaPicha: Sally Hayden/ZUMA/IMAGO

Mbali na suala la usalama, Rais Mohamud ametumia hotuba yake ya uapisho kuomba msaada wa jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na kitisho cha njaa kinachotokana na ukame uliokithiri. Mashirika ya misaada yameonya juu ya nchi hiyo kukaribia kutumbukia katika baa la njaa kutokana na ongezeko la visa vya utapiamlo miongoni mwa watoto katika taifa hilo la pembe ya afrika.

"Ukanda wa mashariki na Pembe ya Afrika unakabiliwa na ukame mkali ambao unatishia maisha ya maelfu ya watu na Somalia inakabiliwa na ukame huo na kuna hofu tayari kwamba baadhi ya maeneo huenda yakakabiliwa na njaa."

Soma pia Rais mpya Somalia apongeza kurudi kwa wanajeshi wa Marekani, ahimiza maridhiano

Umoja wa Mataifa ulisema siku ya Jumatatu kwamba miito mbalimbali ya msaada haijazingatiwa kwa kiasi kikubwa hadi sasa, na karibu nusu ya idadi ya watu nchini humo wanakabiliwa na njaa. Ukame mkali pia umezikumba nchi jirani za Ethiopia na Kenya ambazo viongozi wake walikuwa ni miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla ya uapisho iliyofanyika chini ya ulinzi mkali.

Washirika wa kimataifa wa Somalia wamekaribisha kuchaguliwa kwa Mohamud, huku wengi wakitumai kuwa atahitimisha mgogoro wa kisiasa wa muda mrefu ambao umeivuruga serikali katika kukabiliana na uasi wa Al-Shabaab na ukame mbaya.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ulitoa taarifa kwenye Twitter na kusema kuwa "unampongeza"  Rais Hassan Mohamud na unatarajia kuendeleza ushirikiano na utawala wake katika kuunga mkono kuafikiwa kwa vipaumbele vya kitaifa.