1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUfaransa

Rais Macron afungua mkutano wa kilele wa ufadhili Paris

22 Juni 2023

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amefungua mkutano wa kilele wa ufadhili katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuzungumzia umuhimu wa mabadiliko katika mfumo wa kimataifa wa ukopeshaji fedha

https://p.dw.com/p/4SvTB
Frankreich | Internationaler Gipfel für einen neuen globalen Finanzpakt in Paris
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amefungua mkutano wa kilele wa ufadhili katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuzungumzia umuhimu wa mabadiliko katika mfumo wa kimataifa wa ukopeshaji fedha ili kuhakikisha nchi za kipato cha chini zinaepuka kuchagua baina ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi au umasikini.

Amesema mfumo uliopo wa kimataifa wa ukopeshaji unaoungwa mkono na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, ulionyesha uwezo wake katika miongo iliyopita, lakini hautafaa kabisa katika changamoto za sasa za kiulimwengu.

Napenda kwanza kusisitiza huu ni mkutano wenu. Hii inamaanisha kwamba ni mkutano wa wale wote walio msitari wa mbele kupambana na uharibifu wa sayari hii. Na kile tunachotaka kukiandaa hapa, kwa kweli ni makubaliano mapya yasiyoamuliwa na mtu mmoja, bali yanafanywa na wale wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Na tunapigania mpango wa kwanza wa kukabiliana na umasikini na madhara yake."

Macron ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo anashirikiana na Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley, aliyegeuka kuwa mwanaharakati kinara wa kuangaziwa upya kwa jukumu la Benki ya Dunia na IMF katika zama hizi za mzozo wa kimazingira.