Rais Kenyatta atoa wito wa usalama na umoja Kenya
14 Januari 2019Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla nchini Kenya kudumisha usalama na umoja ili kufikia maendeleo ya kitaifa. Akizungumza kwenye hafla ya Jumapili kanisa la Katoliki, Parokia ya Ridgways kaunti ya Kiambu, Rais Uhuru Kenyatta ameeleza kuwa, ufanisi wa taifa hili unategemea pakubwa utangamano wa watu wake.
Kauli ya Rais Uhuru Kenyatta "Hakuna kitu ambacho hatuwezi tukaafikia na hivyo tutafaulu kwa sababu lengo letu ni kuleta Wakenya wote pamoja." imewiana na zile zilizotolewa na kinara wa chama cha kisiasa chenye ushawishi mkubwa nchini Kenya ODM Raila Odinga na naibu rais William Ruto ambao wamehimiza wanasiasa kujiepusha na siasa za kulipotosha taifa.
Wakizungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwa Philip Anyolo kuwa Askofu mkuu mpya wa kanisa katoliki jimbo la Kisumu, Odinga na Ruto wamesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kuja pamoja kufanikisha maendeleo nchini.
Odinga ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Umoja wa afrika kuhusu maendeleo ya miundombinu, amesisitiza umuhimu wa kuja pamoja ili kutatua changamoto zinazolikabili taifa hili ikiwemo katiba kufanyiwa marekebisho, ili kuimarisha mfumo wa ugatuzi nchini.
"Shida iko wapi nchi yetu hii, tukiwa na katiba mpya lakini bado haifanyi kazi sawasawa”. Amesema Raila.
Kadhalika, Odinga ametoa changamoto kwa kanisa nchini kushiriki mchakato wa kupinga ufisadi ikiwemo kujitenga na viongozi wa kisiasa aliosema huchangia michango ya kanisa ilhali pesa wanazotoa wamezipata kwa njia ya ufisadi. Ameendelea kusema
"Kanisa lizidi kuombea Kenya ili wakenya waweze kupigana na adui mkubwa anayeitwa ufisadi na isikubali kuchukua pesa za ufisadi”
Naye Ruto amesema wakati umefika kwa taifa kujiepusha na siasa za chuki na ukabila.
Naibu rais ameshikilia kuwa, cha kuzingatiwa kwa sasa ni kudumisha undugu na umoja miongoni mwa wakenya wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa wala kabila. "Sisi sote tumekubaliana kwamba siasa ya chuki migawanyiko na ukabila tumewacha nyuma”
Kwenye hafla hiyo, Askofu Philip Anyolo, ametawazwa Askofu Mkuu Mpya wa Kanisa Katoliki jimbo la Kisumu hafla iliyoandaliwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Uzima jijini Kisumu na kuongozwa na kiongozi wa kanisa katoliki nchini Kadinali John Njue.
Anyolo aliyepia Mwenyekiti wa baraza la Ma-askofu wa kanisa katoliki nchini – KCCB, anachukua nafasi hii iliyokuwa inashikiliwa na askofu Zacchaeus Okoth, aliyestaafu baada ya kuhudumu katika nafasi hii tangu mwezi Mei mwaka 1990.
Askofu Anyolo amekua akiongoza kanisa Katoliki jimbo la Homabay.
Mwandishi: Musa Naviye
Mhariri: Iddi Ssessanga