1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Macron aonesha hofu ya mzozo kati ya Uturuki na Ugiriki

13 Agosti 2020

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ataimarisha kwa muda uwepo wa jeshi la nchi hiyo katika eneo la Mashariki mwa Mediterenia kutokana na mzozo wa gesi asilia kati ya Uturuki na Ugiriki

https://p.dw.com/p/3gu3d
Belgien I EU-Gipfel in Brüssel
Picha: picture-alliance/dpa/AFP Pool/J. Thys

Kupitia mawasiliano ya simu na waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis, Macron alielezea wasiwasi wake kuhusu taharuki iliyoko katika eneo hilo. Haya ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa makao makuu ya rais huyo. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa uwepo wa jeshi la Ufaransa utaimarishwa kwa muda katika siku zijazo ili kuangazia hali ilivyo katika eneo hilo na kuonyesha kujitolea kwa taifa hilo katika kuhakikisha uzingatiaji wa sheria ya kimataifa.

Hatua hii itachukuliwa kwa ushirikiano na mataifa washirika wa Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na Ugiriki. Hii leo Mitsotakis ameishukuru Ufaransa kwa ahadi yake hiyo ya kuimarisha uwepo wa jeshi lake katika eneo la Mashariki mwa Mediterania ambapo meli za kivita za Ugiriki na Uturuki zinatishiana kutokana na juhudi za Uturuki za utafutaji nishati katika sehemu ya bahari ambayo Ugiriki inadai kumiliki.

Waziri mkuu wa Ugiriki amemsifu rais wa Ufaransa

Griechenland EU-Spritzenbesuch in Orestiada
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika eneo la mpaka wa Ugiriki na UturukiPicha: picture-alliance/AP Photo/Greek Prime Minister's Office/D. Papamitsos

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa twitter, Mitsotakis alisema kuwa Macron ni rafiki wa kweli wa Ugiriki na pia mlinzi wa maadili ya bara la Ulaya na sheria za kimataifa. Mapema wiki hii, Macron alitoa wito kwa Uturuki kusitisha shughuli hiyo ya utafutaji wa gesi katika eneo hilo la bahari linalozozaniwa hali ambayo imeongeza mvutano na Ugiriki.

Ufaransa ambayo ni mshirikia wa Ugiriki katika shirika la kujihami la NATO na pia katika Umoja wa Ulaya ni taifa lenye uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi katika Umoja wa  Ulaya. Kufanya hali kuwa ngumu zaidi, Uturuki ambayo ni mpinzani mkubwa wa jadi wa Ugiriki katika  kanda hiyo, pia ni mwanachama wa jumuiya ya NATO lakini haina uhusiano mzuri na Ufaransa.

Soma zaidi: Mvutano wa wanachama wa NATO Ugiriki na Uturuki wapamba moto

Ugiriki inadai kuwa sehemu hiyo ya bahari ni milki yake na kutaka meli za Uturuki kuondoka. Uturuki nayo inasema kuwa ina haki ya kufanya utafiti katika eneo hilo. Ugiriki iliweka jeshi lake katika hali ya tahadhari na kutuma meli za kivita katika eneo hilo Kusini mwa Pwani ya Uturuki. Hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki Nikos Dendias amesafiri kuelekea Israeli kuzungumzia suala hilo.