1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biden afanya mkutano na mfalme Abdullah wa Jordan

20 Julai 2021

Rais Joe Biden amekutana na mfalme Abdullah wa pili wa Jordan katika ikulu nchini Marekani katika mkutano wa kwanza kati ya mitatu ya ana kwa ana inayotarajiwa hivi karibuni kati yake na viongozi wa Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/3wjZT
USA I Präsident Joe Biden und König Abdullah II
Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Mfalme Abdullah ambaye mwezi Aprili alikabiliwa na changamoto katika utawala wake kutoka kwa nduguyake kwa baba, mwanamfalme Hamza alikutana na Biden kwa mara ya kwanza tangu rais huyo kuchukuwa hatamu za uongozi mnamo mwezi  Januari. Biden alimtaja mfalme huyo kama rafiki mzuri na mwaminifu.

Biden amewaambia wanahabari kwamba mfalme Abdullah amejitolea siku zote kwa ajili ya Marekani na kwamba Marekani nayo itasimama na Jordan. Alisema anataka kusikia kutoka kwa mfalme huyo kuhusu maendeleo katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba mfalme huyo anaishi katika eneo lenye changamoto nyingi.

Kwa upande wake, mfalme Jordan amesema kuwa taifa lake linakabiliwa na changamoto nyingi katika kutafuta utulivu katika Mashariki ya Kati na kusema taifa hilo na washirika wake wako tayari kutafuta uthabiti katika eneo hilo. Pia ameongeza kuwa Marekani inaweza kumtegemea, taifa lake na washirika wengine wa kanda hiyo.

Mfalme Abdullah amshukuru rais Biden

Mfalme Abdullah alimshukuru rais Biden kwa kusema rais huyo amewaonesha fadhili nyingi . Ameongeza kwamba alikuwa na fursa ya kuona ushirikiano wa rais huyo na babake miongo kadhaa iliyopita. Pia alimshukuru rais huyo kwa kudokeza kuwaunga mkono katika suala la chanjo na kusema ameweka mfano wa kuigwa na wote.

Biden amebadilisha sera ya Marekani kwa Mashariki ya Kati na kurejelea mfumo wa kawaida unaojumuisha uungaji mkono wa suluhisho la mataifa mawili katika mzozo kati ya Israeli na Palestina hatua ambayo mtangulizi wake Donald Trump alijaribu kuiepuka lakini inayoungwa mkono na Jordan. Mfalme Abdullah Jumanne (20.07.2021) anatarajiwa kukutana na naibu rais wa nchi hiyo Kamala Hariss nyumbani kwake  na baadaye kukutana na waziri wa mambo ya nje wa nchini hiyo Antony Blinken.